WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).
Amesema ili kuweza kufanikisha malengo hayo wanahitaji sekta hiyo kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 29, 2019) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Parokia ya Ikwiriri, mkoani Pwani. Ameipongeza Parokia hiyo kwa kubuni mradi wa ujenzi wa shule.
Amesema sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi na wadau muhimu wa sekta hiyo ni pamoja na Serikali, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia na ya kidini, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
Waziri Mkuu amesema kuwa wadau wote hao wamekuwa wakichangia kwa njia mbalimbali katika kuboresha utendaji wa sekta hiyo na kusababisha Serikali kupata mafanikio makubwa sana katika upatikanaji wa huduma za Jamii zikiwemo za elimu, afya na maji.
”Hivi sasa kila Kijiji nchini kina shule ya msingi na ongezeko limefikia idadi ya shule 17,659 zikiwemo zilizo chini ya Kanisa katoliki 204. Pia tumeweza kujenga shule za sekondari katika kila kata ambapo ongezeko limefikia shule za sekondari 4,883 nchi nzima zikiwemo zilizo chini ya kanisa katoliki 266”.
Waziri Mkuu amesema idadi hiyo ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu nchini katika ngazi mbalimbali. ”Hivi sasa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015/2010 tunatekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kutoa sh. Bilioni 24.4 kila mwezi”.
Amesema lengo la Serikali la kutoa kiasi hicho cha fedha kila mwezi ni kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata fursa bila vikwazo na Wilaya ya Rufiji nayo inanufaika, ambapo imetengewa kiasi cha milioni 394.5 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Lengo la Serikali kutoa Elimumsingi Bila Ada ni kuleta ujumuishi kwa kuhakikisha watoto wote hususan wale ambao wanatoka katika familia zisizo na uwezo wanapata haki ya msingi ya kupata elimu.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuongezeka kwa ufaulu wa darasa la saba kumeleta changamoto ya uwepo wa miundombinu ya shule za sekondari hususan kwa kidato cha kwanza ambayo ni kielelezo cha mafanikio ya utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada.
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengoalitumia fursa hiyo kuishikuru Serikalikwa kurejesha hali ya usalama na utulivu katika eneo la Rufiji na Kibiti.
Kardinali Pengoalisema kurejea kwa hali ya utulivu na usalama katika maeneo hayo kumemuondolea mzigo wa kiutendaji uliokuwa ukimuumiza kwa kuwa mapadri aliokuwa akiwapangia katika parokia za huko walikuwa wakisema ‘tumekosa nini’.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment