Waziri Mkuu Afanya Mazungumzo Na Balozi Wa Zambia, Italia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mheshimiwa Balozi Hassan Simba Yahya, ambapo amemtaka akaimarishe mahusiano baina ya nchi zote mbili.

Amekutana na Balozi Yahya leo (Jumamosi, Machi 23, 2019) katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine amemtaka balozi huyo kuhakikisha anaboresha shughuli za Kidiplomasia kati ya Tanzania na Zambia.

Pia, Waziri Mkuu amemtaka akakutane na wafanyabiasha wa Zambia na awahamasishe waje wawekeze katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda. Amesema Balozi huyo anaweza kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji kwa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na Zambia ili kuboresha uchumi.

Kwa upande wake, Balozi Yahya amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha biashara pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Zambia.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Italia waje wawekeze nchini na Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha. Ameyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Balozi Roberto Mengoni.

Akizungumza na Balozi huyo Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni, Dar es salam, Waziri Mkuu amesema Tanzania ipo tayari kuwapokea wawekezaji kutoka kwenye nchi hiyo. “Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2025, hivyo tunawakaribisha wafanyabiashara waje wawekeze”.

Amesema Tanzania iko tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wawekezaji watakaojitokeza kuwekeza nchini wanafanikiwa ili mataifa yote yaweze kufaidika, ambapo Ofisi yake kupitia Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Bibi Angela Kairuki yuko tayari kuwasikiliza na kuwasaidia wawekezaji wote wanaokusudia kuwekeza nchini.

Naye, Balozi Mengoniameishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Italia, hivyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watauendeleza na amesema wapo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda unafanikiwa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments