Waitara: Viongozi Jenganeni Mahusiano Mazuri Na Waandishi Wa Habari Kwani Ni Nguzo Muhimu Kwa Maendeleo Ya Taifa
Naibu waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara amewataka viongozi kutoka ngazi mbalimbali kujenga Mahusiano Mazuri na waandishi wa habari kwani ndio nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Waitara amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wadau wa elimu katika kikao cha Maandalizi ya Mashindano ya Umoja wa Michezo shule za Sekondari ,Tanzania [UMISETA] unaodhaminiwa na Coca cola.
Mhe.Waitara amesema waandishi wa habari wanatakiwa kupewa kipaumbele katika mambo ya Msingi ya Serikali vivyo hivyo katika mashindano hayo ya UMISETA ni vyema vyombo vya habari vikatumika kuibua vipaji vya wachezaji mbalimbali na serikali za mitaa kuwawezesha wanahabari katika kutekeleza majukumu yao kwani ni nguzo muhimu.
“Sio kwamba mpaka aje Mkurugenzi,Waziri No.hata wewe unaweza ,mwanafunzi kafanya vizuri tangaza hiyo,shule za kata zinatoa matokeo mazuri tangaza hiyo.Kuna Ofisi zingine zina pwaya ni mzigo akimwona mwanahabari hata ushirikiano hatoi yeye yupoyupo tu.
"Hivyo katika Mashindano haya tumieni vyombo vya habari,kupitia blogs,redio,magazeti ,vyombo vya habari vyote kuhamasisha michezo.”
Aidha waitara ameagiza Maafisa elimu wilaya ni mikoa kufuatilia somo la michezo kufundishwa kwa nadharia na vitendo,viwanja vya michezo kufufuliwa,kusimamia makusanyo ya fedha za michezo na nyimbo za uzalendo ikiwa ni pamoja na wimbo wa Taifa na wimbo wa Afrika Mashariki kuimbwa hasa kwenye mashindano hayo.
“Unakuta mtu mzima na ofisi yake ukimwambia imba anasingizia ana kikohozi ,tatizo sio kikohozi bali haujui huo wimbo.hivyo tuhamasishe nyimbo za uzalendo kwa Taifa Letu.”
Katika kuboresha na Kutunza Mazingira Mhe.Waitara ameagiza kila mwalimu apande mti mmoja wake shuleni na kila mwanafunzi miti miwili nyumbani na shuleni.
Mkurugenzi Idara ya Elimu Tanzania,Julius Nestory amesema watashirikiana na wadau mbalimbali katika kukuza vipaji vya wanafunzi shuleni huku akipongoza Copa Coca Cola kwa kudhamini Mashindano ya UMISETA.
Kwa Upande wake ,Mkurugenzi wa Mambo ya Umma na Mawasilino ,Coca Cola Haji Mzee Ally amezitaja mikoa atakayoanza katika kuzindua Mashindano ya UMISETA 2019 ni Tabora,Manyara na Ruvuma huku akisema kuwa kutakuwa na mkakati kabambe wa kuzipa zawadi shule zitakazokusanya takataka za plastiki za kampuni yoyote katika kuhakikisha utunzaji wa Mazingira .
Mwenyeji wa Mashindano UMISETA 2019 ni Mkoa wa Mtwara na yanatarajia kuanza mwezi ujao.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment