TFS Yahimiza Watanzania Kuendelea Kutunza Misitu Kwa Ajili Ya Vizazi Vya Sasa Na Vijavyo

Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umewahimiza Watanzania kuendelea kutunza misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho huku ikifafanua ni vema changamoto zilizopo zikatatuliwa kwa majadiliano na hatimaye misitu ibaki salama.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Rasilimali za Misitu Dk.Masota Abel kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo baada ya kumalizika kwa kikao cha majadilano  kati ya maofisa wa TFS na ujumbe wa watu 15 kutoka nchini Ethiopia ambao walikuja nchini Tanzania kujifunza namna nzuri ya utunzaji misitu.

Waethiopia hao wametoka katika taasisi mbalimbali zinazohusika na utunzaji misitu na tafiti katika nchi yao na wakiwa nchini wamepata fursa ya kwenda katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Tanga, Morogoro,Iringa na Dar es Salaam.

 Dk.Masota Abel  amesema ni vema Watanzania wakahakikisha wanatunza misitu iliyopo nchini Tanzania na kufafanua wageni hao kutoka Ethiopia wamefurahishwa na namna TFS inavyotunza misitu , hivyo ametoa ombi kwa Watanzania kuwa sehemu ya kila mmoja kwa nafasi yake kuitunza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho kwa maslahi mapana ya Taifa.

"Ujumbe wangu kwa Watanzania watunze misitu.Tuitunze kwa kufuata taratibu zinazostahili na hata kama kunachangamoto nyingine tutumie nafasi za majadiliano kutafuta ufumbuzi na hatimaye ibaki salama. Tuache kuvamia misitu na kuikata, tuache kufanya shughuli za kilimo maeneo ya hifadhi na misitu kwa ujumla.

"Tunapaswa kufahamu misitu tuliyonayo nchini ni keki ya Taifa na hivyo lazima tuitunze na ilete tija kwa ajili ya kizazi kilichopo sasa na kizazi kinachokuja.Kwetu TFS tutaendelea kuweka mikakati ya kuhakiksha misitu inabaki salama lakini wakati huo huo wananchi nao wanalojukumu kama hilo,"amesema Dk.Abel.

Alipoulizwa changamoto kubwa ambayo TFS wanakabiliana nayo, amejibu ongezeko la watu ni moja ya changamoto kwani wengi hanakosa nishati mbadala ya miti ambayo itakidhi mahitaji kama nchi na kukosekana kwa nishati mbadala imesababisha misitu kuvamiwa na kuharibiwa.

Pia ongezeko la watu limesababisha kuwe na mahitaji makubwa ya ardhi na hivyo wengi kuvamia maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa.Mabadiliko ya tabianchi nayo yanachoche watu kuvamia misitu kwa lengo la kutafuta ardhi yenye rutuba kwa shughuli za kilimo.

Alipoulizwa kwanini Waethiopia hao wameichagua Tanzania , Dk.Arbell amesema kuwa nchi yetu inasifika kwa utunzaji wa mazingira na hivyo wameona ni sehemu sahihi ya kuja kujifunza kuhusu uhifadhi wa misitu .

"Wageni wetu wamekiri na kukubali kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali yetu kupitia TFS katika kutunza misitu, wameeleza namna kile ambacho wamejifunza watakavyokwenda kwao kuweka mikakati itakayowawezesha kuitunza misitu yao.Ethiopa misitu yao imeendelea kuharibiwa .Tunaweza kusema hawana misitu tena.Kwao eneo kubwa limebaki kuwa jangwa, ndio maana wanasema hata asali yao wanafuga katika mabanda .Hivyo hata asali yetu iyabaki kuwa bora na ya asili kuliko ya kwao,"amesema.

Kuhusu ujumbe wa TFS kwa wageni hao waliotoka Ethiopia,Dk.Abel amesema wanashauri waje kuwekeza nchini Tanzania kwani kuna maeneo mengi ya kuwekeza yakiwemo katika sekta ya misitu na viwanda.

 Kwa upande wa wageni hao wamesema Serikali ya Tanzania kupitia TFS wamefanya kazi kubwa na nzuri katika kuhakikisha misitu inatunzwa vizuri na kubwa zaidi ni namna ambavyo kuna utaratibu mzuri wa usimamizi.

Akizungumza wakati akitoa shukrani kwa TFS na Serikali ya Tanzania kwa niaba ya wenzake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Central Ethiopia EV+ & Forest  Wondnossen Tsadik amesema kikubwa ambacho wamejifunza ni namna ambavyo sekta ya misitu inavyoangaliwa kwa ukaribu zaidi.

"Tumeona hapa misitu inasimamiwa na TFS  ambayo iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, hii inafanya kuwepo na ukaribu wa kufuatilia hatua kwa hatua kuhusu uhifahi.Kwetu sisi mambo ya misitu yamechangwa na mambo ya kilimo.Tunaipongeza Tanzania kwa namna ambavyo inasimamia misitu yake,"amesema.

Pia amesema wakiwa katika maeneo mbalimbali ambayo wamekwenda wamepata nafasi ya kukutana na watalaam wa masuala ya misitu pamoja na watafiti wa kada mbalimbali ambapo wamebadilisha uzoefu na wanaamini kila mmoja atakuwa amejifunza kutoka kwa mwingine.

Wakati huo huo Ofisa kutoka Idara ya Ununuzi wa mbegu ICRAF nchini Ethiopia Kedra Mohammed amesema pamoja na mambo mengine amejifunza ukarimu wa Watanzania na kuhusu ziara yao imekuwa ya mafanikio makubwa kwani kuna mengi wamejifunza.


from MPEKUZI

Comments