Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart) Robert Kisena (46) na wenzake watatu umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Kisena na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 19 likiwemo la utakatishaji wa fedha na kuusababishia Mradi wa Udart hasara ya zaidi ya Sh2.41 bilioni.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai leo Jumatatu Machi 25, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba amewataka upande wa mashtaka kuhakikisha shauri hilo wanalifuatilia ili upelelezi ukamilike kwa wakati.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 3, 2019 itakapokuja na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Mbali na Kisena washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na raia wa China, Cheni Shi (32).
Katika mashtaka yao, yamo pia ya kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa pamoja na shtaka la wizi wakiwa wakurugenzi.
Pia wanakabiliwa na mashtaka manne ya utakatishaji fedha, kughushi manne, kutoa nyaraka za uongo manne, mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la kusababisha hasara kwenye mradi huo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment