CUF Kuwapeleka Mahakamani Waliochoma Bendera na Kadi za CUF

Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Tanga, kimefungua kesi mahakamani kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria waliokuwa wanachama wa chama hicho waliohamia Chama cha ACT- Wazalendo kwa madai ya kuchoma bendera na kadi za chama hicho.

Hayo yalibainishwa jana kwenye kikao maalumu kilichoshirikisha wanachama na madiwani wa chama hicho ambao walikuwa na ajenda ya kujadili mustakabali wao baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhamia ACT Wazalendo mapema wiki hii.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF Taifa, Masoud Mhina, alisema dhumuni la kikao hicho ni kujitathmini na kuchukua hatua kwa wale waliochoma bendera na kadi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mhina alisema kikao hicho cha kamati tendaji pia kimetoa tamko la kumtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Tanga, Rashidi Jumbe, kuhakikisha mali zote za CUF  alizokuwa anazishikilia anazirudisha kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yake.

Alisema miongoni mwa mali za chama hicho zinazoshikiliwa na Jumbe ni pamoja na pikipiki tatu, spika, samani za ofisi na mafaili.

 “Tunaheshimu maamuzi yao ya kujiunga na chama mbadala, lakini kuhama kwao hakuhalalishi kuondoka na mali za chama chetu, mali zote za CUF zirejeshwe kwa mustakabali wa chama hicho,” alisema.


from MPEKUZI

Comments