CCM Zanzibar Yawaonya ACT- Wazalendo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya viongozi wa siasa wanaotumia vibaya uhuru wa demokrasia kuhatarisha amani ya nchi.

Chama hicho kimewataka viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF ) kutotumia mipasuko na migogoro yao kuhatarisha amani na kwamba Wazanzibari kwa ujumla hawapo tayari kuingia katika machafuko ya kisiasa kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache.

Akizungumza  jana katika hafla ya kukabidhi basi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Magomeni mjini Unguja,  Jamal Kassim Ali kwa chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Sadala maarufu ‘Mabodi’, alisema CCM itaendelea kusimama imara na kupaza sauti inapoona baadhi ya watu wachache wanavunja sheria za nchi kwa makusudi bila ya kujali misingi ya utu na haki za binadamu.

Alisema baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi kujiunga na ACT-Wazalendo wameshuhudia vitendo vya uvunjifu wa sheria kwa makusudi vinavyofanywa na wanachama wa ACT Wazalendo.

Katika maelezo yake, Mabodi aliongeza kuwa wanachama wa ATC-Wazalendo wamefanya uharibifu wa mali za CUF ikiwemo kuchoma nguo za chama hicho, bendera, kung’oa samani zilizoko katika ofisi mbalimbali sambamba na kutumia dini katika harakati za chama hicho.

“Mambo yote hayo ni ishara za wazi zinazochochea vurugu na migogoro baina ya wanachama wa vyama hivyo viwili, zinazoweza kuingiza nchi katika athari kubwa ya machafuko.

“Tunavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki mapema, kwani dhana ya amani na utulivu wa nchi haviuzwi katika maduka kama bidhaa bali imeletwa na sera bora za CCM.

“Wito wangu kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini tuwaongoze na kuwaelekeza mambo mema wanachama wetu, kwa kuwajengea mazingira ya kuamini ushindani wa sera badala ya siasa za ovyo na machafuko”, alisema Naibu Katibu Mkuu.

Alisema nchi zilizoingia katika machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe zilianza taratibu, huku taasisi na mamlaka zenye dhamana ya ulinzi na usalama zikipuuza kuchukua hatua badala yake mataifa hayo yamejikuta yakingia katika vita.

Credit: Mtanzania


from MPEKUZI

Comments