Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru apandishwa mahakamani na Kusomewa Mashitaka 8

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kulthum Mansoor amefikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akikabiliwa na makosa nane ikiwemo la utakatishaji fedha wa shilingi bilioni 1.4.

Kulthum amepandishwa kizimbani leo Ijumaa Machi 29, 2019 akitokea kituo cha polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam ambako alikuwa mahabusu toka jana Alhamisi alipokamatwa kwa tuhuma hizo.

Mshtakiwa amekosa dhamana kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpatia. 

Jana, Rais Magufuli akizungumza Ikulu mara baada ya kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola alisema kuna mkurugenzi mmoja wa makao makuu Takukuru aliwauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake, lakini anashangaa hajapelekwa mahakamani hadi sasa.

“Wala sijapata taarifa kwamba hizo fedha amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu. Wafanyakazi wanaumia, wanalalamika pembeni.

“Amewadanganya kwamba ana viwanja Bagamoyo, lakini mpaka leo hawajapewa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kashfa hiyo iliibuliwa tangu Balozi Mlowola alipokuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Suala hili lilianza tangu wakati wa Balozi Valentino, nikamuuliza huyu mbona harudishi fedha au hapelekwi mahakamani, akawa na kigugumizi, sasa na wewe usiwe na kigugumizi kwa sababu nafasi za ubalozi zimeisha.

 “Ndiyo maana huwa najiuliza hawa Takukuru huwa ni kwa ajili ya watu wengine, wao ‘hawaji-takukuru’ humo humo ndani?” alihoji. 


from MPEKUZI

Comments