Serikali Haitomuacha Salama Mtumishi Yeyote Atakaekula Fedha Za Umma Kwa Masilahi Binafsi

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amesema Serikali haitosita kumchukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria  mtumishi wa umma yeyote atakaebainika kula fedha za umma ambazo zinatolewa na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, mara baada ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo ili kujiridhisha na utekelezaji wa mpango huo.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa umma wote nchini kuwa waaminifu na waadilifu katika kutumia vema fedha za umma ambazo malengo yake ni kuwaletea maendeleo wananchi hususani wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ametoa wito kwa watumishi wa umma kubadilika na kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu, akitoa mfano wa fedha zaidi ya shilingi milioni 457 ambazo zilitolewa na Serikali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ambazo zilitumika kinyume na utaratibu, na kuongeza kuwa, halmashauri hiyo ililazimika kuzirejesha baada ya Serikali kubaini ubadhirifu huo na kuamuru zirejeshwe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab R. Kawawa amemueleza Dkt. Mwanjelwa kuwa, baada ya kuwachukulia hatua watumishi wabadhirifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, mapato ya Halmashauri hiyo yaliongezeka kutoka milioni 400 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia milioni 760 kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2018 na kuongeza kuwa, kutokana na hatua iliyochukuliwa anaamini mapato ya Halmashauri hiyo yataongezeka na inawezekana yakafikia bilioni moja katika  kipindi  hiki cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi, 2019.

Mhe. Kawawa ameahidi kuendelea kuwashughulikia ipasavyo watumishi wote wanaohujumu mapato ya Serikali katika wilaya yake kwani atahakikisha mapato yanaongeza, na kufafanua kuwa pasipo shaka wapo watumishi wachache wanaohujumu vyanzo vya mapato na kufanya ubadhirifu hivyo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuendelea kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wote waliobainika kujihusisha na kuhujumu mapato na kushiriki katika ubadhirifu wa fedha.

Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) anaendelea na ziara ya  kikazi kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma Mkoani Pwani, mpaka sasa  ameshakutana na watumishi katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ambapo amewataka watumishi hao kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kuzingatia weledi katika utendaji kazi.


from MPEKUZI

Comments