Mwili wa Kijana Frank Kapange (22) aliyefariki zaidi ya miezi nane na siku 26 na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, umechukuliwa na ndugu kwenda kuzikwa katika kijiji cha Syukula katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya baada Mahakama kuamuru mwili huo kuzikwa.
Akizungumza hospitalini hapo, Msemaji wa Familia, Julius Kapange amesema kupitia mahakama mbalimbali mkoani Mbeya waliomba mwili ufanyiwe uchunguzi ili kujua sababu za kifo cha kijana wao ambaye anadaiwa kufariki kwenye mazingira ya kutatanisha lakini waliamuriwa kuuzika mwili huo ndani ya wiki moja vinginevyo Halmashauri ya Jiji ingezika.
Shangazi wa marehemu Sophia Kapange amesema hawakususia mwili bali walitaka kujua sababu za kifo cha mtoto wao ndiyo maana walikuwa wakifuatilia mahakamani ili haki itendeke lakini imekua tofauti na matarajio yao huku Mama mzazi wa marehemu akidai kifo cha mwanae kimekuwa pigo kwake kwani alikuwa akiendesha familia kwa kufanya biashara ndogo ndogo katika Soko la Sido.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Godlove Mbwanji amesema wameamua kusamehe gharama zote za kutunzia mwili wa marehemu ili fedha ambazo waliziandaa zikatumike kwenye msiba.
Frank alifariki Juni 4, 2018 huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido jijini Mbeya alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi hivyo ndugu waligoma kumchukua na kwenda kumzika.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment