Mradi Wa Soko La Kisasa Manispaa Ya Morogoro Wamkuna Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji

Na Peter Haule, WFM, Morogoro
Halmashauri zote nchini zimetakiwa kujifunza kutekeleza miradi ya Kimakakati inayopatiwa ruzuku na Serikali, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa thamani halisi ya mradi wa Soko la kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 17 hadi kukamilika kwake inaonekana.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko la Kisasa katika Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro wenye lengo la kuzifanya Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kujitegemea kimapato.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Kama ipo halmashauri iliyopewa fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kuwekeana mkataba na Serikali na bado inashindwa kufuata makubaliano ya mkataba ijifunze kutoka Manispaa ya Morogoro.

“Ukilinganisha na miradi mingine ya kimkakati niliyoikagua katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huu ni wa mfano, zipo halmashauri ambazo zimepewa fedha halafu zinarudi tena kuangalia upya mikataba ambayo waliwekeana saini na Serikali jambo ambalo linatia mashaka, tuje tujifunze kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa nini ameweza kwenda na wakati ulio katika mkataba”alisema Dkt. Kijaji.

Alipongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 30 japo walitakiwa kufikia asilimia 40 katika kipindi hiki kutokana na changamoto ya kujaa maji na kuutaka uongozi wa Manispaa hiyo kukamilisha ujenzi ndani ya kipindi cha miezi mitano ili wafanyabiashara waanze kulitumia soko hilo.

“Mapato ya Soko hili yataongezeka kutoka Shilingi bilioni moja, kwa mwaka hadi Sh. bilioni 4 kwa kuwa idadi ya wafanyabiashara itaongezeka kutoka 400 kwa sasa hadi 900 na huduma zingine zitatolewa kama Benki” alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya kuanzisha miradi ya kimkakati kwa manufaa ya watanzania itatimia kupitia mradi wa Soko la Kisasa la Manispaa ya Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo, ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo Wilayani kwake, kwa kuwa soko lililokuwepo lilijengwa mwaka 1953 hivyo kuwa na miundombinu mibovu iliyosababisha wananchi kuwa na magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu, hivyo mradi huo si tu utaongeza mapato na kuweka mandhari nzuri, lakini pia utaimarisha afya za wananchi.

Naye Meya ya Manispaa ya Morogoro  Bw. Pascal Kihanga, alisema kuwa waliwaahidi wananachi kusimamia ujenzi wa Soko hilo jambo ambalo linatekelezwa kwa juhudi kubwa, hivyo kufikia mwezi Septemba mwaka huu mradi utakabidhiwa kwa Serikali na wafanyabiashara wote walioondolewa kupisha mradi na  wengine watarudi.

Mhandisi wa Mradi huo Antonio Mkinga, amesema kuwa mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa, kwa kuwa mpaka sasa hakuna vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia utekelezaji wake.

Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 17 zilizokidhi vigezo vya kutekeleza jumla ya miradi 22 ya kimkakati nchini kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 147 ambapo Manispaa hiyo ilipata mradi huo wa soko la kisasa litakalogharimu shilingi bilioni 17.


from MPEKUZI

Comments