Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewataka upande wa mashtaka kuja na maelezo ya kutosha kuhusu kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake watano upelelezi wake umefikia hatua gani.
Yusuf na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Candid Nasua kuieleza Mahakama hiyo, jana Jumatatu Februari 25,2019 kuwa imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
"Wakili wa Serikali aliyekuwa anaendesha shauri hilo hayupo hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alidai Nasua.
Hakimu Simba alisema, “kesi hiyo ipo mikononi mwenu tangu mwaka 2016, hatutaendelea kuwavumilia mnatakiwa kumfikishia ujumbe wakili wa serikali huyo kuwa siku tutakapokutana tena mje na majibu sahihi.
Hakimu Simba aliliahirisha shauri hilo hadi Machi 11, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.
Katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh392.8 milioni bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment