Finland yaipongeza Tanzania vita dhidi ya Rushwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Timo Soini.amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli za kupambana na rushwa na kusimamia uwajibikaji.

Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye yupo nchini Finland kwa ziara ya kikazi ya siku mbili tarehe 25 na 26 Februari 2019.

Kwenye mazungumzo yao, Mawaziri hao wamesisitiza umuhimu wa Tanzania na Finland kuboresha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, uwekezaji, mafunzo ya ufundi, ajira kupitia sekta ya misitu, ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa kwa kuzingatia usawa, pamoja na kuwajengea uwezo wanawake na watoto.

Aidha, Mhe. Soini  alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi na mchango mkubwa katika usuluhishi wa migogoro inayozikabili baadhi ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Hivyo, walikubaliana kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ikiwa ni pamoja na biashara ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, na matishio ya ugaidi.

Kabla ya mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Sampo Suihko, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha OMNIA Espoo ambaye alieleza utayari wa Taasisi yake wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa kutoa mafunzo ya elimu ya ufundi yanayoendana na soko la ajira.

Mhe. Mahiga pia alifanya mazungumzo na Mhe. Matti Ahtisaari, Rais Mstaafu wa Finland na Mwanzilishi wa Taasisi ya Utatuzi wa Migogoro. Mhe. Ahtisaari aliipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya katika utatuzi wa migogoro kwenye nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na kusihi kuendeleza jitihada hizo kwa ustawi wa Dunia nzima.

Vilevile, Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Bw. Jukka Kallio, Makamu wa Rais wa Helsinki. Katika mazungumzo hayo, uongozi wa Bandari ya Vuosaari umeahidi kushirikiana na uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania katika kuboresha mifumo ya kidigitali (Digitalization) itakayoongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Katika kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchini, Mhe. Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara (Business Finland) na Makampuni makubwa ya kibiashara nchini humo. Wafanyabiasha hao walipongeza jitihada zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na  waliahidi kuwekeza na kushawishi makampuni mengine kuona umuhimu wa kuwekeza nchini Tanzania.

Mhe. Waziri anahitimisha ziara hiyo kwa kufanya mazungumzo na Bi. Anne-Mari Virolainen, Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland; Bw. Mauri Pekkarinen, Naibu Spika wa Bunge la Finland, Bw. Juhan Damski, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi  ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya nchini Finland na baadaye kuzungumza na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Finland.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
26 Februari 2019


from MPEKUZI

Comments