Benki ya NMB imetoa Sh. bilioni 500 kwa ajili ya kusaidia wakulima na wafugaji wa viwanda vidogo na vikubwa ili kuinua uzalishaji wa maziwa nchini ikiwamo sekta ya kilimo.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa sekta hizo, Meneja Mwandamizi katika Idara ya Mikopo na Kilimo, Isack Nyangaro, alisema lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kwenda na sera ya awamu ya tano ya kutaka nchi ya viwanda, ndio maana wametoa fedha hizo.
Alifafanua kuwa mpaka sasa wametoa Sh.trilioni 2.7 kwa jamii hiyo na kwa sekta ya kilimo wametoa Sh. bilioni 148, kupitia dirisha la watalaam la kilimo hadi kufikia 2019.
Alisema lengo lao ifikapo mwaka 2020 wawe wametoa fedha hizo kwa wafugaji na wakulima ili kuhakikisha wanainua sekta hiyo.
Kwa upande wa Serikali, Waziri wa Mifugo, Luhaga Mpina, alisema anashangazwa kuona Tanzania inazidiwa na Kenya katika uzalishaji wa maziwa ilhali nchi ina malisho bora kuliko nchi hiyo.
Alisema Kenya hivi sasa inazalisha maziwa lita bilioni 5.2, huku Tanzania ikizalisha lita bilioni 2.4, wakati ina malisho bora kuliko nchi nyingine.
Mpina alisema hakuna sababu ya Tanzania kuzidiwa uzalishaji na Kenya wakati kuna kila kitu, huku akiwataka kuhakikisha wanafikia uzalisha kama ilivyo Kenya, ikiwamo kusimamia suala la soko.
Alisema wao kama Serikali wako pamoja katika kuhakikisha mifugo yote inakua salama ili iweze kutoa maziwa mengi kama ilivyo kwa nchi nyingine za Ethiopia na Kenya.
Alisema wamefunga mitambo ya kupima na kugundua magonjwa ya mifugo na wameanza kubaini na kuzuia mlipuko wa magonjwa.
Alisema wanazalisha madawa na chanjo huku akisema wanaagiza dawa kwa mfumo ambao si wa gharama kubwa ambao hauwezi kuleta athari yoyote nchini.
"Tunadhibiti kuhakikisha hakuna chanjo isiyo salama kwa mifugo yetu lengo ni kusonga mbele katika ufugaji," alisema Mpina.
Alisema gharama za chanjo haziwezi kuwa kubwa huku akiwataka wafugaji kujitokeza kwa sababu watapata dawa kwa bei nafuu ikiwamo chanjo sahihi.
Alifafanua zaidi kuwa ndani ya mwaka mmoja watahakikisha chanjo zote 11 zinapatikana hapa nchini ili kuwarahisishia wafugaji kufuga kisasa zaidi bila wasiwasi wa magonjwa.
Aidha, alisisitiza benki kutoa mikopo kwa wafugaji ili kuhakikisha wanakwenda sawa katika uzalishaji wa maziwa hapa nchini.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment