Afisa Utumishi Mkuranga Aonywa Kutumia Cheo Chake Vibaya Kuomba Rushwa Ya Ngono Kwa Watendaji Wa Vijiji

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amemuonya Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Bw. Valintine Mbai ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri hiyo kuacha tabia mbaya  ya kutumia cheo chake kuomba rushwa ya ngono kwa Watendaji wa Vijiji katika Halmashauri hiyo na kumtaka afisa huyo kubadili mwenendo wake haraka iwezekanavyo.

Onyo hilo amelitoa wilayani Mkuranga, wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kuanza kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo ili kujiridhisha na utekelezaji wake.

Akizungumza na watumishi hao, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, ni aibu kwa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia maadili ya kiutumishi kutumia madaraka yake vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono toka kwa Watendaji wa Vijiji jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma.

Amemtaka afisa huyo kuacha tabia hiyo na kujirekebisha maramoja ili awe mfano bora kwa watumishi anaowasimamia kimaadili.

Pi amemtaka, afisa huyo kuwa na heshima kwa wakuu wake wa kazi akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ili kutengeneza mazingira mazuri ya kiutendaji.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ametoa angalizo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Juma Abeid kutowatetea watumishi wasio waadilifu na badala yake awachukulie hatua za kinidhamu hata kama ni marafiki zake.

Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameendelea kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini akiwa wilayani Mkuranga na kutoa wito kwa watumishi wote wa umma kuhakikisha wazingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.


from MPEKUZI

Comments