Serikali Yalaani Mauaji ya Watoto Njombe

Serikali imelaani mauaji ya kinyama ya watoto watatu wa familia moja yaliyotokea mkoani Njombe na kusema kuwa tukio hilo halitapita bure na inataka iwe fundisho kwa watu wenye roho za kinyama wanaotekeleza mauaji ya watoto wadogo hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamadi Masauni wakati wa mazishi ya watoto watatu Godliver, Giliad na Gasper Nziku wote wa familia moja ambao wamefariki dunia kwa kuchinjwa na kutupwa maeneo tofauti, katika Kijiji cha Ikando, Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe

”Tukio hili haliwezi kupita bure, tunataka iwe fundisho kwa wale wote wenye roho za kinyama, taaarifa ambazo nimeshazipata mpaka sasa jeshi la polisi limeshawapata watuhumiwa na hatua nyingine zinaendelea ili kuhakikisha mtandao wote unaohusika na hili unashughulikiwa,”amesema Masauni

Aidha, katika mazishi ya watoto hao, ndugu mmoja wa familia aliyesoma taarifa ya marehemu hao, Josephine Gaudensi amesema kuwa mtu aliyehusika na mauaji hao aliwachukuwa watoto watatu kati ya watano waliokuwa katika familia hiyo huku wazazi wakiwa hawapo.

Hata hivyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amesema kuwa mpaka sasa vifo vya watoto wadogo vilivyotokea mkoani Njombe ni jumla ya watoto 6 huku akiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana katika ulinzi wa familia ili kuweza kuepukana na janga hilo.


from MPEKUZI

Comments