Wema Sepetu Aitwa Kuhojiwa Tena

Bodi ya filamu imesema alichokifanya Wema Sepetu kutangaza filamu ya ‘Saa Mbovu’ sio sahihi kwa kuwa bado hawajamfungulia kujishughulisha na kazi za filamu.

Wema alitangaza filamu hiyo  katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, filamu ambayo kacheza na Aunt Ezekiel wakiwa kama wahusika wakuu.

Mtendaji wa Bodi hiyo, Joyce Fisoo, amesema wamesikitishwa na kitendo hicho na tayari wamemuita kumhoji kwa nini amefanya hivyo na kwa nini asichukuliwe hatua.

Amesema kanuni za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza namba 156 za Mei 2011, kifungu cha 50 kinaeleza kuwa kwa yeyote atakayetenda kosa kwa kukiuka masharti ya kanuni hizo atatozwa faini isiyopungua Sh5 milioni.

Amebainisha kuwa mbali na kumuita Wema, pia walikihoji kituo cha Azam kujua kwamba wao ndio walimpa kazi ya kutangaza filamu hiyo, ambao walikana na kudai kuwa wanatangaza kupitia mitandao yao.

Kuhusu kumalizika kwa adhabu yake, amesema bado yupo katika uangalizi hadi Aprili mwakani, ambapo amepewa kazi tatu kubwa za kufanya na endapo wataridhika watatangaza kwa umma ni hatua gani watazichukua dhidi yake.


from MPEKUZI

Comments