Serikali imekusanya makusanyo ya ndani katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza (Julai – Novemba), 2018 Sh. trilioni 7.37 sawa na asilimia 88.9 ya makadirio ya Sh. trilioni 8.30 katika kipindi hicho.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema hayo jana wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa bajeti ya serikali, mjini Dodoma.
Alisema katika kipindi hicho, mapato ya kodi yalifikia Sh. trilioni 6.23 ikiwa ni asilimia 88 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 7.04 kwa kipindi hicho.
Aidha, alisema mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh. bilioni 936.03 sawa na asilimia 21 zaidi ya lengo la Sh. bilioni 775.36 na mapato ya halmashauri yalifikia Sh. bilioni 203.8 sawa na asilimia 61 ya lengo.
Dk. Mpango alisema ongezeko la mapato yasiyo ya kodi limetokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji kwenye taasisi, mashirika na kampuni kulikoiwezesha serikali kupata michango na gawio stahiki kutoka kwenye uwekezaji wake; kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye wizara na idara zinazojitegemea kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato uitwao Government Electronic Payment Gateway (GePG) na kati ya Julai 2017 hadi Novemba 2018, jumla ya taasisi za serikali 325 zimetumia mfumo huo kukusanya maduhuli.
Akizungumzia jitihada za kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara, alisema serikali kupitia Sheria ya Fedha 2018/19 ilipunguza ada na tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa wananchi. Miongoni mwa ada na tozo zilizopunguzwa ni pamoja na za mazingira, OSHA, FIRE, TBS, TFDA na tozo kwenye madini ya chumvi.
Kuhusu changamoto ya ukusanyaji wa mapato, alisema ni pamoja na ukwepaji wa kodi; mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti pale wanapofanya manunuzi na wafanyabiashara kutoa risiti pale wanapofanya mauzo; na wigo mdogo wa kodi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment