Polisi Dodoma Wakanusha Mtoto Kufungiwa Kabatini

Wakati binti wa kazi akieleza jinsi mwanaye mwenye umri wa miezi mitano alivyofungiwa kabatini na  mwajiri wake mkoani Dodoma kwa muda wa miezi sita, Jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini.

Binti huyo wa miaka 15, jana Desemba 30, 2018 akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alidai kufanyiwa ukatili kwa kupigwa na kufanyishwa kazi hadi usiku wa manane  na bosi wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu na kwamba amekuwa akimwambia amfungie hadi usiku mtoto wake na kila alipovunja masharti alikumbana na kipigo.

Leo Desemba 31, 2018 polisi mkoani Dodoma imekanusha madai ya mtoto  huyo kufungiwa kabatini kama inavyodaiwa, lakini wamekiri binti huyo kushambuliwa na mwajiri wake.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto amesema polisi wamefanya upekuzi katika nyumba ya mwajiri wa binti huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu, Anitha Kimako na kubaini hakuwa na kabati nyumbani kwake.

"Kesi ya shambulio ipo na ameshambuliwa kweli na ndiyo maana tunamshikilia. Anashikiliwa kutokana na usalama wake kwani kelele za watu ni nyingi, ila hili suala la kuwekwa mtoto kabatini halipo," amesema Muroto.

Amesema uchunguzi wa kina unafanyika na kwamba lazima mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Medali afikishwe mahakamani.


from MPEKUZI

Comments