Pendo Adolph Manyama (29) na watoto wake wawili, wakazi wa Kola katika Manispaa ya Morogoro, wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuungua na moto uliyosababishwa na kulipuka kwa jiko la gesi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Wilbrod Mutafungwa, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 26, mwaka jana, saa 10:30 jioni , maeneo ya Kola, Manispaa ya Morogoro.
Mutafungwa alisema siku hiyo mtoto wa mama huyo aliyejulikana kwa jina la Angela Baltazar (4) alifungua mtungi wa gesi na kusababisha gesi kujaa ndani ya nyumba hiyo.
“Wakati mtoto akifungua mtungu huo, mama yake ambaye alikuwa Mwalimu wa shule ya Msingi Forest, bila kujua aliingia ndani na jiko la mkaa na kusababisha moto kulipuka na kumuunguza yeye na watoto wake wawili, jambo lilosababisha vifo vyao,” alisema.
Aidha, Kamanda Mutafungwa aliwataka wananchi kuwa waangalifu wakati wote wanapokuwa wanatumia vyombo hivyo vya majumbani, ili kuepusha ajali mbalimbali za moto kutokea.
Mmoja wa jamaa wa karibu na familia hiyo, alielezea tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita wakati mume wa mama huyo, Baltazar Kineneko (37) akiwa mkoani Arusha kikazi.
“Ilikuwa majira ya usiku mama akiwa anapika kibarazani kwenye jiko la mkaa mtoto wa miaka minne aliingia ndani na kuchezea jiko la gesi, gesi ikawa inavuja.
Mtoto alipofungua mlango kutoka nje mvutano wa gesi na mkaa ulisababisha mtungi wa gesi kulipuka hadi juu na kutoboa gypsum.
“Mama aliingia ndani kumuokoa mtoto, lakini alitoka akiwa anaungua mwili mzima. Mtoto wake mwingine wa miaka sita
aliyekuwa nje anacheza alipoona mamaye anatoka ndani na mdogo wake huku wakiwa wanaungua moto alikimbia kumkumbatia mama yake naye akaanza kuungua,” alieleza jamaa huyo.
Ndugu huyo alisema mama na mtoto mdogo walikufa papo hapo, mtoto mkubwa alisafirishwa kwa ndege kwenda Nairobi nchini Kenya kwa matibabu baada ya hali yake kuonekana mbaya.
Hata hivyo, jamaa huyo alisema baba wa mwanamke aliposikia kuwa mwanaye na mjukuu wamekufa alipata mshtuko naye akafa hapo hapo, alizikwa jana mkoani Morogoro.
“Baba wa mtoto yaani mume wake yule mama katoka leo (jana) Nairobi, ili kesho (leo) amzike mke na mwanaye kisha arudi Nairobi kumuuguza mwanaye aliyebaki, lakini usiku wake akiwa safarini alipigiwa simu kuwa mtoto aliyemwacha
Nairobi naye kafariki,” alieleza mtu huyo.
Alisema baba huyo yupo katika wakati mgumu hiyo anawaomba watanzania wamuombee, ili aweze kulikabili jambo hilo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment