Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepigwa marufuku kufunga maduka na biashara za watu kwa kisingizio cha kutolipa kodi, badala yake imetakiwa kukaa meza moja na wafanyabiashara ili kujadiliana nao.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa agizo hilo jana wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya Serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.
“Utaratibu wa kumfungia biashara mfanyabiashara anayedaiwa kodi ili kumshinikiza alipe sasa usitishwe mara moja, isipokuwa kwa wakwepa kodi sugu na hapo lazima kuwe na kibali cha kamishna wa mkuu wa TRA, nataka mjikite katika kutoa elimu siyo vitisho,” alisema Dk Mpango.
Waziri huyo alikemea matumizi mabaya ya lugha, vitisho na ubabe dhidi ya walipakodi wenye historia nzuri akitaka yasipewe nafasi na itakapothibitika mtumishi wa TRA amekwenda kinyume awajibishwe kwa kuzingatia tararibu za kiutumishi.
Dk Mpango alisema hata Rais John Magufuli amekwishaagiza utaratibu wa kufungia maduka usitishwe alipofungua kikao kazi cha TRA Desemba 10, hivyo amri hiyo inapaswa kutekelezwa.
Kiongozi huyo aliagiza TRA kujikita katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waone faida na thamani ya kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao na akawataka kupambana na wakwepa kodi hasa katika maeneo ya bandari bubu ambako alisema dawa yao ni kuwalipisha kodi na kutaifisha bidhaa zilizokwepa kulipiwa.
Dk Mpango alisema hali ya maisha ya Watanzania imeendelea kuimarika hasa waliopata ajira na katika shughuli za uchumi zinazokua kwa haraka kama ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege ambao wengi wamejenga nyumba bora.
Alisema ukuaji mzuri wa uchumi uliisaidia Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato na kugharamia uboreshaji wa huduma za jamii katika zahanati, elimu, dawa, maji na kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuusambaza vijijini.
Dk Mpango alisema mabadiliko yaliyofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Juni 2017 yaliweka masharti ya uendeshaji wa maduka ya kubadilishia fedha ambapo yamesababisha zaidi ya nusu ya maduka hayo kufutwa kwa kutokidhi vigezo.
“Tuliweka masharti kuwa kiwango cha chini cha mtaji wa maduka yaliyoko daraja A kiongezeke kutoka Sh100 milioni hadi 300 milioni na daraja B kutoka Sh250 milioni hadi 1 bilioni, hivyo zoezi la usajili limeendeshwa na tulikuwa na maduka 297, lakini tumetoa leseni kwa maduka 109 ndiyo yamekidhi vigezo,” alisema
Waziri Mpango alisema sekta ya benki imeendelea kuimarika na kutengemaa ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kunachotakiwa kisheria ambapo mitaji ya benki ukilinganishwa na rasilimali zao ni asilimia 16.3 wakati kiwango kinachotakiwa ni asilimia 10.
Waziri alisema katika kipindi cha Januari hadi Novemba, sekta hiyo ilipata faida ya Sh285.4 bilioni ikilinganishwa na Sh317 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka jana wakati mikopo chechefu iliendelea kushuka hadi kufikia asilimia 9.7 ya mikopo yote mwezi Septemba 2018 kutoka asilimia 12.8 iliyorekodiwa Desemba 2017.
Waziri Mpango alisema shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu katika kipindi cha Julai hadi Novemba ambapo Dola ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2,276 ikilinganishwa na Sh2,235 katika kipindi kama hicho 2017.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment