Askofu aonya misaada ya Wazungu Inayotaka Tukubaliane na USHOGA

Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi amewataka watanzania kuepukana na misaada inayotokana na ushoga kutoka mataifa ya nje.
 
Aidha, amewataka kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo adhabu ya viboko kuanzia nyumbani hadi shule hali inayowafanya kujengeka kikatili kwenye makuzi.
 
Cheyo ametoa wito huo katika Kanisa la Mabatini Kata ya Mbalizi Road Jijini Mbeya katika ibada ya mbaraka kwa wanandoa kumi ibada iliyovuta hisia za watu wengi Jijini Mbeya.
 
Hata hivyo ameiasa serikali na jamii kwa ujumla kupinga vitendo vya ushoga kwani ni kinyume na maadili ya Kikristo.
 
“Taifa liepukane na misaada inayotokana na ushoga kutoka mataifa ya nje kuwakuwa ni kinyume na maadili ya dini ya kikristo, hivyo tuupinge kwa nguvu zote,”alisema.
 
Hata hivyo, Askofu Cheyo alisema vitendo vya ukatili vimekuwa vikiongezeka katika jamii vikiwemo vya ubakaji na ulawiti katokana na watoto kufanyiwa ukatili wangali wadogo.
 
Aidha alipendekeza kuondoolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kwani hali hiyo inawafanya watoto kuwa wakatili hata ukubwani.
 
“Ndugu zangu Watanzania sasa hivi tumeshuhudia vitendo vya kikatili dhidi ya watoto kutokana jamii kushindwa kutoa malezi bora kwa watoto wetu”alisema Cheyo.
 
Pia Cheyo amesikitishwa na wanandoa kushindwa kuvumiliana katika ndoa na baadhi ya jamii kuingilia migogoro ya ndoa, amesema migogoro hiyo inapaswa kumalizwa na wanandoa wenyewe na si vinginevyo.

Ameiasa jamii kuheshimu ndoa kwani ndoa ni taasisi huru inayopaswa kujiendesha yenyewe badala ya watu kutoka nje.
 
Akitolea mfano amesema hata migogoro ya ndoa kupelekwa kwa wachungaji au mabalozi si sahihi kwani hata wao wana matatizo yao kwa kuwa nao ni binadamu.
 
Aliwahimiza wanawake kuwa wasafi na kuwataka wanaume kuwaheshimu wanawake.


from MPEKUZI

Comments