Wizara Ya Maliasili Na Utalii Yatenga Mamilioni Kuwezesha Ufugaji Nyuki Kisasa

NA LUSUNGU HELELA-GEITA
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) imetenga kiasi cha Sh700milioni kwa ajili ya kuwawezesha wananchi  kufuga  nyuki kwa njia ya kisasa kwa mikoa nane.

Kauli hiyo imetolewa leo Mbogwe katika mkoa wa Geita na Naibu Waziri wa Maliasili na Utaii, Mhe,Constanine Kanyasu  wakati  akizungumza na wananchi  kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

 Ametaja baadhi ya   wilaya katika mkoa wa Geita zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni wilaya ya Ushirombo pamoja na Mbogwe.

Kufuatia hali hiyo, Mhe. Kanyasu  amezitaka wilaya hizo kujiepusha na ukataji miti ovyo kwa  vile nyuki ni rafiki wa mazingira  badala yake zijikite zaidi  katika kupanda miti.

Akizungumzia kuhusu fungu hilo, Mhe, Kanyasu amewataka wakazi wa wilaya hizo wajiunge  katika vikundi  ikiwa ni moja ya vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji wa pesa hizo  kwa ajili ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa.

Aidha,Naibu Waziri huyo amesema  wafugaji hao wataokakuwa wamejiunga katika vikundi hivyo watapatiwa elimu ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa pamoja na kuwezeshwa pesa zitakazotumika kwa ajili ya kununulia  mizinga ya kisasa itakayosaidia kuzalisha mazao ya nyuki yatakayokidhi soko la kimataifa,

Ameongeza kuwa baadhi ya pesa hizo zitatumika katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyowasaidia wafugaji hao  kuchakata na kufungasha mazao ya asali yenye viwango bora duniani.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kanyasu amewahakikishia wananchi hao kuwa tayari Wizara imepata soko la uhakika la  asali watakayoizalisha.

Ameongeza kuwa licha ya nchi ya  Tanzania kusifika katika uzalishaji  wa asali kwa wingi,,Wafugaji walio wengi wamekuwa wakifuga nyuki kimazoea

Kufuatia hali hiyo amesema Wizara imedhamiria kuleta mapinduzi katika uzalishaji wa mazao ya nyuki kwa kuwawezesha wananchi kufuga kisasa hali itakayosaidia wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhifadhi misitu.


from MPEKUZI

Comments