Serikali Ya Norway Yaridhishwa Na Ukarabati Wa Vituo Vya Kuzalisha Umeme Nchini

SERIKALI ya Norway imefurahishwa na jitihada zilizofanywa na serikali nchini katika kusimamia fedha walizotoa mwaka 1995 kugharamia miradi ya ukarabati wa vituo vya kuzalisha umeme vilivyopo hapa nchini.

Akizungumza leo baada ya kutembelea kituo cha New Pangani Falls, katika ziara yake ya kukagua miradi wanayoifadhili, Waziri wa Maendeleo nchini Norway Nicolai Astrup, alisema walitoa fedha hizo kwa serikali kutokana na uhusiano uliopo baina ya mataifa hayo ikiwemo usimamizi mzuri uliofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Waziri huyo pia alisema kuwa serikali yake imeongeza mkataba wa kusaidia uwekaji wa nishati ya umeme katika maeneo ya vijiji kutoka mwaka 2020-2021 baada ya kuridhika na usimamizi mzuri uliofanywa katika ukarabati wa vituo hivyo.

“Nipo hapa Pangani Falls, Norway na Tanzania wanahusiano muda mrefu, nimekuja kufuatilia matokeo ya msaada tuliotoa mwaka 1995, kwa vituo vya kuzalisha umeme ‘Hydro Power Plants’,” alisema.

Baadaye akizungumza na wananchi wa mji wa Bagamoyo wilayani Korogwe Waziri huyo alisema kwamba nishati ya umeme ni muhimu katika maendeleo ya wananchi katika kufanya shughuli zao za kiuchumi na kwamba serikali yao itanedelea kushirikiana na Tanzania kusaidia nishati hiyo.

Serikali ya Norway ilitoa kiasi fedha za Kimarekani dola milioni 126 awamu ya kwanza na kisha awamu ya pili ya ukarabati wa vituo vya kuzalisha umeme vya New pangani Falls, Kidatu, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Mtera ukarabati uliomalizika Aprili mwaka huu walitoa jumla ya shilingi bilioni 21.

Awali akizungumza Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu alisifu juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Norway kuwekeza kwenye sekta ya nishati kwa nchi hatua ambayo imewezesha maeneo mengi kunufaika na huduma hiyo muhimu.

Licha ya kufanyia ukarabati lakini pia walishiriki katika ujenzi kwa kutoa zaidi ya asilimia 42 pamoja na Serikali ya Sweeden kwenye ujenzi wa kituo hicho hatua ambayo imesaidia kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Alisema serikali ya Norway ni wadau wakubwa kwenye utekelezaji wa umeme vijijini na mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa iliyopata fursa ya uwepo wa vijiji vinavyofadhiliwa na katika mradi wa umeme vijijini ujazilizi.

“kwa kweli kama Naibu Waziri naishukuru sana Serikali ya Norway kwa jitihada kubwa wanazofanya kwa uwekezaji kwenye sekta ya nishati katika nchi yetu sio suala la kupeleka umeme vijijini pekee lakini wamekuwa wakiwekeza kwenye sekta za mafuta na gesi”Alisema Naibu Waziri Mgalu.

Aliongeza kuwa licha ya uwekezaji wao katika maeneo hayo lakini pia katika sekta ya nishati jadidifu kwa kuangalia maeneo yaliyopo mbali kuweza kuyawekea miundombninu ya umeme ambao umesaidia kuchochea kazi ya ukuaji wa maendeleo kwenye baadhi ya maeneo.

“Sisi tunaona katika hili wametupa fursa na wamehaidi kuendelea kushirikiana na serikali kwenye maeneo mbalimbali hasa ya vijijini kuhakikisha yanapata nishati ya umeme na wamefadhili mpaka 2021 kuona vijiji vinapata umeme”Alisema.


from MPEKUZI

Comments