Polisi Dar Yaua Majambazi Hatari 6

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam mnamo tarehe Novemba 29, 201 katika maeneo ya Ubungo UFI kupitia Kikosi Kazi Maalum cha Kupambana na Ujambazi, lilifanikiwa kuwaua majambazi sita na kukamata silaha moja aina ya AK 47, risasi 11, kitambulisho chenye namba OP 0216239 kwa jina la THEOPHILI MANIRAKIZA mkazi wa Rukana Rugombo nchini Burundi na kitambulisho cha kazi kinachotumiwa na kikundi cha CNDD-FDD chenye jina hilo la Theopili Manirakiza katika majibizano ya risasi.

Majambazi hao waliuwawa baada ya mtego uliowekwa na askari kufuatia taarifa za watuhumiwa watatu waliokuwa wamekamatwa (WILLY IRAKOZES@Commando raia wa Burundi, JEAN MUGISHA raia wa Burudi na Mtanzania OMARY NASSORO) waliokuwa na bunduki tatu aina ya AK47 na magazine 08, risasi 217 na mabomu ya kutupa kwa mkono 8, ambao walipanga tarehe 29/11/2018 majira ya saa 10 :30 alfajiri kufanya tukio la kumpora mfanyabiashara aliyekuwa akisafiri kuelekea Morogoro akisadikiwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha.

Ofisi ya Kamanda wa Polisi, Kanda maalum inaeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuwepo kwa matukio ya uhalifu yaliyotokea huko Mabibo External tarehe 03 Nov 2018 ambapo mfanyabiashara wa TIGOPESA/MPESA aliporwa Tshs. 50 milioni na huko Tegeta tarehe 15 Nov 2018 mfanyabiashara raia wa China ambaye aliporwa Tshs. 10 milioni.

Aidha jambazi huyu WILLY IRAKOZES@Commando amekuwa akitafutwa kwa kufanya matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa katika tukio la kuvamia Benki ya NMB Temeke ambapo aliua askari wawili (02) na raia.

Tarehe 15 March 2011 akiwa anashikiliwa kituo cha Polisi Kagongwa Kahama kwa makosa mbalimbali yeye na wenzake walitoroka baada ya kuwaua askari polisi 02 na kutoroka na silaha mbili aina ya AK47.

Aidha matukio mengine waliyoshiriki ni pamoja na kuteka mgodi wa Tulawaka Geita mwaka 2011, kuvamia maduka ya kubadilishia fedha za kigeni huko Zanzibar, Mwaka 2012 walivamia kituo cha mafuta huko Kagera na kufanya mauaji, Pia walivamia maduka yaliyopo karibu na kituo cha Polisi Chato na hivyo kukishambulia kituo ili kurahisisha uporaji ambapo walipora Tshs,3 milioni na mwaka 2010 walivamia mgodi wa Nyamongo na kufanya mauaji ya askari 01 na kujeruhi wengine.

LAZARO B. MAMBOSASA-SACP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAAM
29/11/2018


from MPEKUZI

Comments