Zitto Kabwe Akamatwa na Jeshi la Polisi

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anashikiliwa na jeshi la polisi kwaajili ya mahojiano juu ya mauaji ya Polisi na raia yaliripotiwa wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu imesema kuwa kiongozi huyo amekamatwa na Polisi wa kituo cha Osterbay jijini Dar es salaam.

"Kiongozi wa Chama, ndugu Zitto Kabwe amekamatwa na Polisi wa Kituo cha Polisi Oysterbay muda huu kwa maelezo kuwa anakwenda kuhojiwa juu ya mauaji ya Polisi na raia yaliyotokea kwenye Kijiji cha Mpeta, wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, mauaji ambayo Zitto alitaka Jeshi la Polisi liyatolee maelezo katika mkutano wake na Wanahabari juzi Jumapili, Oktoba 29, 2018", amesema Shaibu.

Jana, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018 kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno amesema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.


from MPEKUZI

Comments