Waziri Mkuu Alivyoweka Wazi Uozo Wa Askari Kushiriki Kwenye Biashara Ya Magendo

TANGU Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, imekuwa ikitilia mkazo  ukusanyaji kodi kupitia vyanzo mbalimbali vya serikali.

Mapato ya kodi yanayokusanywa yamewezesha Serikali kugharamia miradi mikubwa ya kiuchumi iliyopo kwenye mkakati wa kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa viwanda.

Hata hivyo licha ya jitihada hizo ukwepaji wa kodi na biashara za magendo zinayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu mipakani, wamelifanya Taifa limekuwa linapoteza mapato yatokanayo na kodi.

Serikali mara kwa mara kupitia vyombo vya dola imekuwa ikiendesha msako kuwakamata watu wanaokwepa kodi na kuwafikisha katika vyombo vya sharia.
Cha kustaajabisha baadhi ya askari waliopewa dhamana hiyo ndiyo wanashirikiana na wafanyabiashara katika kusindikiza bidhaa za magendo.

Hali hiyo imebainika mwezi huu wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kagera.

Waziri Mkuu alibaini kuwepo kwa baadhi ya askari polisi pamoja na watumishi wa forodha kwenye mipaka Tanzania na nchi za Uganda na Rwanda, wakishiriki kuvusha magendo.

Jambo hilo la kusikitisha lilionyesha kumkera Waziri Mkuu, hivyo kuwaagiza viongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanaongeza umakini katika usimamizi wa mipaka hususan kwa watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Jumapili, Oktoba 7 mwaka huu, baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilaya Kyerwa, Waziri Mkuu alimuagiza  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Olomi, awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi jirani. Miongoni mwa polisi hao yupo aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Justin Joseph.

“Askari polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi ya jirani kupitia njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma.” alibanisha.

Waziri Mkuu alisema ni jambo la hatari kama askari polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo, hivyo ameagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka. "Marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na polisi msishiriki katika butura.” alitoa msisitizo.

Katika kuonesha kuwa Serikali imekerwa na vitendo hivyo vya polisi kujihusisha na biashara za magendo, ikiwemo kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwenda nchi jirani kwa njia hiyo, Rais Dk. Magufuli, Oktoba 8, mwaka huu aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Olomi.

Askari wengine alioagiza wasimamishwe kazi ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa, Justin Joseph, Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Kyerwa, Evererist Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyerwa, Robert Marwa.

Viongozi hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya zao la kahawa katika wilaya ya Kyerwa pamoja na tuhuma nyingine.

Waziri Mkuu alisema kuna askari polisi wa wilaya hiyo walikwenda kufanya kikao na wafanyabiashara wa nchi jirani na kupanga mikakati ya kuvusha bidhaa mbalimbali ikiwemo kahawa kwa njia ya magendo ambapo walipewa ng’ombe wawili.

Alisema mbali na askari polisi pia, baadhi ya watumishi wa idara ya forodha nao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo hususan katika mipaka ya Mulongo na Mutukura.

Baada ya kuchukizwa na biashara za magendo zinazofanywa na baadhi ya watumishi katika wilaya hiyo ya Kyerwa, Oktoba 10 mwaka huu, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa wilaya hiyo wajipime.

Alisema Serikali imewapeleka katika wilaya ya Kyerwa ili wakafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi na si vinginevyo na kwamba watumishi wote watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika awamu hii.

Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera, Adam Ntogha, kumsimamisha kazi Ofisa wa Forodha katika mpaka wa Mulongo, Peter Mtei kwa tuhuma za kujihusisha na biashara za magendo.

“Biashara za magendo zinafanyika bila ya wao kuchukua hatua, mnatia aibu yaani hakuna kazi inayofanyika. Viongozi wa wilaya ya Kyerwa mjipime wenyewe, mialo mingi katika wilaya yenu inatumika kwa biashara ya magendo na butura.”

Aliongeza kuwa katika mwalo wa Mulongo ulipo kwenye eneo ambalo  Tanzania inapakana na nchi za Uganda na Rwanda, biashara za magendo na butura zinafanyika na hakuna kiongozi wanaochukua hatua.

Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TRA asiwahamishe watumishi wabovu kutoka kituo kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwa kuwa huko anakowapeleka wanakwenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha Serikali mapato.

Alitolea mfano mtumishi wa mamlaka hiyo, Mtei ambaye alihamishiwa kituo cha Mulongo akitokea kwenye kituo cha Mtukura kilichopo katika mpaka wa Tanzania na Uganda kwa tuhuma za kuchua rushwa na kushirikiana na wafanyabiashara wa butura.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema mtumishi huyo tayari alishapewa barua ya uhamisho kwenda katika kituo cha forodha cha Rusumo miezi minne iliyopita hadi sasa hajahama na anaendelea na biashara za magendo ambapo Agosti 5, mwaka huu anadaiwa kupitisha mzigo wa magendo uliobebwa kwenye gari aina ya fuso yenye za usajili T 957 AXF mali ya Erasto Muga.

“Meneja TRA msimamishe kazi Mtei, hatuwezi kuwa na watumishi wabovu alafu nyie mnawahamisha vituo ili wakaendelee kuharibu eneo lingine. Mnajua mkakati wa Serikali hii ni kudhibiti rushwa hivyo hatuwezi kuvumilia suala hili.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Meneja wa TRA wa mkoa wa Kagera afanye ukaguzi kwenye vituo vyote vya forodha katika mkoa huo pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Biashara ya magendo kwa muda mrefu imekuwa ikiikosesha Serikali mapato kwa kuwa fedha zinazotakiwa kulipwa kodi na kuingia kwenye mfuko wa Serikali zimekuwa zikiishia mikononi mwa watendaji wasiokuwa waaminifu.

Jambo hilo kwa kiasi kikubwa limekuwa likirudisha nyuma mipango ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo kama uboreshaji wa huduma za jamii na ujenzi wa miundombinu.

Wananchi pamoja na wafanyabiashara wanatakiwa watambue kuwa wanawajibu wa kulipa kodi na kwamba tayari Serikali imeshatoa maelekezo kwa Jeshi la polisi kuwakamata wote wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 29, 2018.


from MPEKUZI

Comments