Waziri Mkuu Aagiza Eneo La Kiomoni Litathminiwe.....Ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanancho juu ya kutoridhishwa na fidia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamuagizaMthamini Mkuu wa Serikali Bibi. Evelyne Mugasha kwenda katika Kata ya Kiomoni kufanya tathmini ya ardhi ya wananchi ili kubaini thamani halisi ya maeneo hayo ili wananchi waweze kufidiwa.

Hatua hiyo inakuja baada ya wananchi hao kumlalamikia Waziri Mkuu kuhusu kutoridhishwa na fidia ya maeneo yao yaliyochukuliwa na kampuni ya Neelkanthinayomiliki kiwanda hicho cha kuzalisha chokaa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Oktoba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kiomoni katika mtaa wa Kiomoni wilayani Tanga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga.

Alisema atamtuma Mthamini Mkuu aende kubaini nani anadai nini na anamiliki nini ili atoe kibali cha ulipwaji ili muwekezaji aweze kupewa kibali cha kuwalipa fidia yao.”Tunataka jambo hili liishe kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kila kitu kiwe kimekamilika na hakuna mwananchi hata mmoja atakayepoteza haki yake ya msingi.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambayo viwanda mbalimbali vya saruji nchini vinategemea kwa kupata malighafi, hivyo alimpongeza muwekezaji na kumshauri aongeze uzalishaji kadiri anavyoweza.

Alisema wawekezaji katika sekta ya viwanda ni muhimu kwa sababu wanaunga mkono mkakati wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.

Alisema fursa ya uwepo wa kiwanda hicho utawezesha kukuza uchumi Taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu kiwanda kitakapokamilika kitatoa ajira ya watu zaidi ya 2,000 wakiwemo wakazi wa eneo hilo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Bw. Thobias Mwilapwa Mkinga leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) akutane na wananchi wa kijiji hiko na kusikiza kero mbalimbali zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili, ambapo aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kwenda kwa wananchi.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 31, 2018.


from MPEKUZI

Comments