Wawili Watiwa Mbaroni Kwa Kumtorosha Kada wa CCM Anayetuhumiwa Kumbaka Mwanafunzi Jijini Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunawashikilia watu wawili wanaofahamika kwa majina ya Mgassa Carlos @ Jeremiah, miaka 42, mkazi wa Bulele na Jafari Swalehe, miaka 57, kwa kosa la kumtorosha kusikojulikana mtuhumiwa aitwaye Hasan Bushangama, @ Ngalinda, miaka 43, katibu Mwenezi wa CCM kata ya Buhongwa, aliyekuwa amekamatwa na Polisi kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili jina tunalihifadhi, mwenye umri wa miaka 17, shule ya sekondari buhongwa, baada ya kumchukulia mdhamana Polisi, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo la kumpa mimba mwanafunzi liliripotiwa kituo cha Polisi miezi miwili iliyopita ambapo baada ya kuripotiwa polisi tulifanya msako mkali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.  

Aidhaa wakati tukiendelea kumshikilia mtuhumiwa kituoni kwa mahojiano zaidi, watuhumiwa wawili tajwa hapo juu walifika kituoni kumchukulia mdhamana huku wakiwa wamekamilisha taratibu zote kisheria. 

Pia kwasababu ni haki yake kisheria mtuhumiwa kupewa dhamana kulingana na kosa analotuhumiwa nalo basi polisi tulimpatia dhamana.

Ndipo wakati polisi tulipomhitaji mtuhumiwa kituoni ili tuweze kukamilisha taratibu za kumfikisha mahakamni hakufika na alipotafutwa hakupatikana na baadae tulipata taarifa kuwa ametoroka.  

Baada ya kupata taarifa hizo tulifanya msako mkali wa kuwakamata wadhamini wake wote wawili na kufanikiwa kuwakamata na tayari tumewafikisha mahakamani.

Katika tukio la pili; Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunamtafuta mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Zephilin Michael, miaka 43, katibu mwenezi wa CCM kata ya Mkolani, maarufu muuza kahawa, kwa tuhuma za kumlawiti kijana mmoja jina tunamhifadhi huko kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Amani iliyopo Mtaa wa Mkolani Wilayani Nyamagana , kitendo ambacho ni kosa la Jinai.

Tukio hilo limetokea tarehe 26.10.2018 majira ya saa 11:30hrs, hii ni baada ya mtuhumiwa kumuajiri kijana huyo kwenye kazi ya kuuza kahawa mtaani kisha alimpangishia chumba namba tatu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Amani ili pindi anapotoka kuuza kahawa awe anafikia hapo. 

Ndipo tarehe na majira tajwa hapo juu mtuhumiwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kumuuliza mhudumu kama kijana wake yumo ndani ya chumba chake ndipo alielezwa na mhudumu yupo ndani na yeye alimfuata humo chumbani huku mhudumu akiendelea na shughuli zake.

Aidha baada ya muda mchache kupita ilisikika sauti ya mtu akipiga kelele toka ndani ya chumba hicho na baadae watu walipochungulia kupitia dirishani walimuona mtuhumiwa akimlawiti kijana huyo. 

Ndipo walipomtaka afungue mlango aligoma na baadae alifungua na kutoroka na kijana huyo pia alitoroka kisha wananchi walitoa taarifa polisi. 

Polisi tunaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wote wawili ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa wakazi wa jiji na Mkoa wa Mwanza tukiwataka waache tabia hizo mbaya za ubakaji  na ulawiti kwani ni kosa kisheria na endapo mtu yeyote atabainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. 

Vilevile tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikianao kwa Jeshi la Polisi kwa kutupa taarifa za uhalifu na waalifu ili waweze kukamatwa na  kufikishwa katika vyombo vya sheria.


from MPEKUZI

Comments