Waganga wafawidhi wametakiwa kujadili sababu ya vifo vinavyotokea kwenye hospitali zao ili kuzifanyia kazi changamoto hizo na kurudisha taarifa Wizara ya Afya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu Wizara ya Afya, Dk. Otilia Gowelle, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waganga wafawidhi nchini, Dodoma jana.
“Waganga wafawidhi mnatakiwa kukaa vikao vya utabibu kujadili tiba pamoja na kujadili kifo cha kila mgonjwa kujua changamoto iliyotokea na kuipatia ufumbuzi na kuandikia taarifa kuondokana na vifo hasa vinavyotokana na uzazi,” alisema Dk. Gowelle.
Aliwataka wataalamu wa tiba kuzingatia vikao vya tiba na kufanyia kazi changamoto au maboresho ili kuzitolea taarifa na kuzitatua pamoja na kushirikisha wadau wengine.
Dk. Gowelle aliwataka pia waganga wafawidhi kuweka mifumo ya ufuatiliaji wagonjwa na kupokea malalamiko katika hospitali zao kufanya maboresho ya huduma za afya wanazozitoa na kuchukua hatua zinazostahili.
“Kupitia kikao hiki, nawataka mkae kama timu na kuandaa mipango kazi ya kuanza kushughulikia kwa ukamilifu yale yote yaliyobainika katika taarifa hiyo.
“Lengo ni kuondokana na kero wanazokabiliana nazo wananchi wanapokuja kupata huduma katika hospitali zenu,” alisema Dk. Gowelle.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment