Wafanyakazi Watano Wa NEMC Wafikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma Za Kughushi Saini Ya Waziri Januari Makamba

Wafanyakazi watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi, ikiwamo kula njama na kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka hayo jana Jumatano Oktoba 31, 2018 na wakili wa Serikali, Faraja Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Akisoma mashtaka hayo, Nguka alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh 160 milioni.

Wakati washtakiwa hao wakisomewa mashtaka hayo,  mshtakiwa mwenzao, ofisa mazingira wa Nemc, Magori Wambura (38) ambaye hakuwepo mahakamani, imetolewa hati ya kumkamata ili asomewe mashtaka yanayowakabili wenzake.

Washtakiwa waliosomewa mashtaka ni ofisa mazingira wa Nemc, Deusdith Katwale (38) mkazi wa Ubungo Msewe, mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi (33) mkazi wa Ubungo Msewe, sekretari wa baraza hilo, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisa Mwaruka Mwaruka (42) mkazi wa Ukonga Mombasa na ofisa mazingira NEMC, Lilian Laizer (27) mkazi wa Ukonga Mombasa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa  kati ya Septemba  27, 2016 na April Mosi, 2018 Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  Oktoba 17, 2017 Dar es Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba, 2017 Dar es Salaam kwa nia ovu walighushi saini ya Makamba katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la nne,  mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba  2017 katika ofisi za Nemc Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 cha Oktoba 17, 2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la tano, washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 27 na Aprili 6 ,2018 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh160 milioni toka kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na Nemc kitendo ambacho si kweli.

Katika shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba27, 2016 na Aprili 6, 2018 Dar es Salaam waliisababishia Nemc hasara ya Sh160 milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mashtaka ya uhujumu uchumi Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza hadi Mahakama Kuu.

Washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14, 2018.


from MPEKUZI

Comments