Vigogo waliojilimbikizia mashamba makubwa ya mkonge Kuanza Kuchunguzwa

Vigogo waliojilimbikizia mashamba makubwa ya mkonge wako hatarini kupokwa kutokana na mpango wa serikali kuyafanyia ukaguzi wa kuwabaini walioyatelekeza bila kuyaendeleza.

Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akisema serikali itaanza kufanya ukaguzi mashamba yote ya mkonge nchini kwa lengo la kubaini yale ambayo hayafanyi vizuri ili wayafute na kupatiwa watu wengine watakaokuwa na uwezo wa kuyaendeleza.

Aidha, Lukuvi ameijia juu Bodi ya Mkonge Tanzania kwa kushindwa kusimamia vizuri kampuni zinazozalizasha zao hilo ambapo mengi yao uendeshaji wake hauna tija kwa kuwa hayatoi ajira za kutosha kwa wananchi wanaozunguka eneo husika sambamba na kuikosesha serikali mapato.

Lukuvi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na uongozi wa kampuni ya kuzalisha mkonge ya LM Investments Ltd iliyopo katika kijiji cha Ndungu Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro wakati akikamilisha ziara yake ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Hai, Moshi na Same.

“Mashamba mengi ya mkonge hapa nchini uendelezaji wake hauna tija, hauridhishi na wamiliki wake wanahodhi tu maeneo jambo linaloikosesha serikali mapato, huku wengine wakitumia mashamba hayo kukopea fedha katika benki,” alisema Lukuvi.

Alisema pamoja na kuwapo Bodi ya Mkonge ambayo ina jukumu la kusimamia uendeshaji zao hilo, lakini imeshindwa kufanya kazi ipasavyo, hivyo kusababisha makapuni ya kuzalisha mkonge kufanya yanavyotaka.

“Kama bodi ya Mkonge wameshindwa kuchukua hatua kwa wale wasiofanya vizuri katika uzalishaji wa mkonge, basi sisi kama Wizara ya Ardhi tutafanya ukaguzi kwa mashamba yote ya mkonge ili tubaini wale wasiofanya vizuri na tuwanyang’anye na tuwapatie watu wengine wenye uwezo,” alisema Lukuvi.

Kauli ya Lukuvi inafuatia kutoridhishwa na uendeshaji wa Shamba la Mkonge la Ndungu lenye ukubwa wa hekta 1,230 linalomilikiwa na Kampuni ya LM Investments Ltd. 

Shamba hilo limekuwa na mgogoro na wananchi wa vijiji vitatu vya Ndungu, Gonja Mperani na Msufini. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya LM Investments Ltd, Allan Chellangwa, shamba hilo limekuwa likizalisha wastani wa tani 30 mpaka 50 kwa mwezi na lengo ni kuzalisha tani 50 kwa mwezi huku wafanyakazi 24 wakiwa wameajiriwa.

Maelezo hayo yalimshtua Lukuvi ambaye alisema uwiano wa hekta 1,230 na ajira za watu 24 hauendani na kueleza kuwa lengo la serikali kutoa mashamba makubwa kwa wawekezaji ni kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kupata mapato kupitia kodi na kusisitiza serikali haiwezi kuacha shamba lenye ukubwa huo kutoa ajira za watu wachache tu.

Wenyeviti wa vijiji vya Msufini, Gonja Mperani na Ndungu waliiomba serikali kuwapatia ekari 100 kila kijiji ili ziwasaidie katika shughuli zao. Mwenyekiti wa Kijiji cha Msufini, Omar Mganga, alimueleza Lukuvi kuwa kijiji chake kimekuwa na uhaba wa ardhi jambo linalosababisha wananchi wa eneo hilo kukosa maeneo ya makazi na ya kuzikia.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vyote vitatu, Lukuvi aliwaeleza kuwa moja ya kazi ya serikali ni kuondoa kero, kulinda wawekezaji na kutetea wanyonge na kufafanua kuwa jukumu la serikali siyo kufukuza wawekezaji, ila ni kutaka kuwa na wawekezaji wenye tija, watakaoleta teknolojia mpya pamoja na kuongeza pato la taifa.

Katika kutatua mgogoro huo, Lukuvi aliamuru vijiji hivyo vitatu vipatiwe jumla ya hekta 300 kutoka hekta zinazomilikiwa LM Investments Ltd 1,230 ambapo hekta 71 ni zile zilizoongezwa tofauti na makubaliano ya umilikishwaji mwaka 1998 na nyingine zitatoka ndani hekta zinazomilikiwa na kampuni ambapo kila kijiji sasa kitapatiwa hekta 100 jambo lililopokelewa kwa furaha na wananchi wa vijiji hivyo.


from MPEKUZI

Comments