Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mkutano wa pamoja wa 16 wa mawaziri wa biashara wa nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika Brussels. Ubelgiji.
Kwenye mkutano huo Tanzania ilisisitiza azma ya kutosaini mkataba wa EPA.
Mbali na mkutano huo, Profesa Kabudi alishiriki mkutano wa 21 wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara wa ACP.
Taarifa iliyotolewa jana, ilisema mikutano hiyo miwili ilitanguliwa na mkutano wa makatibu wakuu wa nchi za ACP wanaosimamia masuala ya biashara.
Ilisema katika mkutano huo, Tanzania ilisema mkataba wa EPA hauwezi kuwa nguzo au chachu ya maendeleo kama ilivyo katika malengo yake kwa kuwa hautoi fursa kwa nchi za ACP kukuza sekta ya viwanda na biashara.
Ilisema badala yake mkataba huo una sura ya misaada kutoka EU kwenda ACP na umelenga nchi za ACP kuwa soko kuu la bidhaa za EU.
Taarifa hiyo ilisema mkataba huo una vikwazo vingi visivyo vya ushuru ambavyo husababisha nchi za ACP zishindwe kufanya biashara ya bidhaa na huduma na nchi mbalimbali za EU.
“Tanzania ilirejea msimamo wake wa awali wa kutosaini mkataba wa EPA hadi hapo utakapoboreshwa na kuwa na sura ya ushirikiano wa maendeleo ya uchumi.
“Baada ya Tanzania kutangaza msimamo wake, baadhi ya nchi nyingine za ACP ziliunga mkono hoja hii na kuhamasisha nchi nyingine zaidi za ACP zichukue msimamo wa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema katika mikutano hiyo Profesa Kabudi aliongozana na Naibu Katibu Mkuu, Biashara na Uwekezaji kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Edwin Mhede na wataalamu wengine waandamizi kutoka Wizara ya Viwanda, Viashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Brussels.
Tanzania ni miongoni mwa wanachama wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) tangu mwaka 1975. Nchi hizo za ACP zimekuwa na majadiliano na Umoja ya Ulaya (European Union – EU) kwa lengo na kukuza ushirikiano miongoni mwao.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment