Shahidi adai Mshahara na Posho za mhasibu Takukuru Ilikuwa Sh 334,175,332.05.

Ofisa  Uchunguzi Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Naza Alawi (43), amedai mahakamani kwamba  aliyekuwa  Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai, alifukuzwa kazi baada ya kukutwa na hatia ya kukosa uaminifu.

Kipato cha mshtakiwa huyo cha mshahara na posho katika kipindi chote cha ajira kilikuwa   Sh 334,175,332.05.

Shahidi huyo alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akingozwa na Wakili wa Serikali Vitalis Peter, shahidi alidai majukumu yake kusimamia dawati la mishahara, kuandaa malipo, kulipa kodi mbalimbali na kutunza kumbukumbu ya daftari la watumishi waliokopa.

“Gugai alianza kazi Juni mwaka 2001 hadi Julai mwaka 2016 utumishi wake ulipokoma baada ya kufukuzwa kwa kukosa uaminifu.

“Alikutwa na mali ambazo hakuzitolea tamko kwenye tamko la mali, nilipewa maelekezo na mhasibu ya kuchambua mishahara ya Gugai kuanzia alipoanza kazi hadi alipofukuzwa, “alidai.

Alawi alidai mshahara wa Gugai alipoanza kazi Julai mwaka 2001 ulikuwa Sh 152,630, Februari mwaka 2004 ulipanda na kufikia Sh 191,822.15 ,hadi anafukuzwa kazi mshahara wake ulikuwa Sh 4,417,838.

Anadai posho za mazingira magumu Julai mwaka 2001, alikuwa analipwa Sh 45,000, Machi mwaka 2008 alilipwa Sh 341,784 na mpaka anafukuzwa posho hiyo alikuwa analipwa Sh 1,362,800.

Shahidi alidai posho ya matibabu alilipwa Sh 150,000 kuanzia Agosti mwaka 2006 hadi Juni mwaka 2003 na posho ya nyumba ilikuwa Sh 92,858.40 Julai 2007 na Mei mwaka 2009 ilipanda na kuwa Sh 142,450.

“Kwa kipindi chote cha ajira Gugai alilipwa   mshahara wa Sh 218,916,859.65, posho ya mazingira magumu  Sh 99,944,099.50, posho ya matibabu Sh 12,450,000 na posho ya nyumba j Sh 2,864,372.90.

“Jumla ya kipato chote cha Gugai katika kipindi chake cha ajira ni Sh 334,175,332.05,”alidai Alawi.

Shahidi huyo pia alichambua mshahara na posho za mke wa Gugai, Lina Francis, aliandikia ripoti ambayo alitaka kuitoa mahakamani kama kielelezo.

Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alipinga kuwasilishwa   ripoti hiyo akidai kwamba muhusika hakuwapo  mahakamani.

Baada ya hoja hiyo mahakama iliahirisha kesi hadi leo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi baada ya kujiridhisha kuhusu sheria inasemaje katika mazingira hayo.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine  ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Gugai anakabiliwa na shitaka la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambako alitenda kosa hilo kati ya January 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa   akiwa  Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh bilioni 3.6 ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa huku akishindwa kuzitolea maelezo.


from MPEKUZI

Comments