Mwakyembe Aagiza Wamiliki Na Wahariri Wa Gazeti la Tanzanite Wahojiwe

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb), amesema habari iliyochapishwa na gazeti la kila siku la Tanzanite la leo Jumatatu tarehe 29 Oktoba, 2018 lenye habari zenye tuhuma za kisiasa dhidi ya Viongozi kadhaa, haziakisi msimamo wa Serikali na ameagiza mmiliki na Bodi ya uhariri ya gazeti hilo waitwe mara moja Idara ya Habari (MAELEZO) kujieleza kuhusu msingi wa habari hiyo.

Dkt. Mwakyembe ametoa ufafanuzi huo leo mchana, mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuelezea kushtushwa kwake na mwenendo wa gazeti hilo kuchapisha habari zinazoibua tuhuma za kisiasa dhidi ya baadhi ya Viongozi nchini, wakiwemo Wabunge na kusababisha taharuki kubwa katika jamii.

Gazeti la Tanzanite linatolewa na kampuni ya CZ Information and Media Consultant LTD ya Dar es Salaam na leo katika toleo lake Na. 254 limeandika katika ukurasa wake wa mbele  habari yenye kichwa kinachosomeka “Vigogo 14 hatari kwa nchi watajwa” ambayo inawataja viongozi kadhaa wa kisiasa na wafanyabiashara.



from MPEKUZI

Comments