DC Mjema Aibua Ufisadi wa Viwanja 1125 Ilala, Dar

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ameibua ufisadi wa viwanja 1,125 vilivyotakiwa kupewa wakazi wa Kipawa waliohamishwa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kiamataifa wa  Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika kata 35 za nanispaa hiyo jana, Mjema alisema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ilipima viwanja 5,096 kwa ajili ya kuwahamisha wananchi waliotakiwa kupisha lango la tatu la uwanja huo (terminal III).

Alisema kati ya viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya wanananchi hao ni viwanja 3971 pekee vilivyogawiwa.

Alisema mpaka sasa wakazi 514 waliohamishwa katika eneo hilo hawajapata viwanja huku TAA ikitafuta viwanja vingine kwa ajili ya kuwapatia.

“Suala hili tumelikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuvitafuta viwanja 1125,” alisema Mjema.

Alisema mgogoro huo una sura tatu, moja ikiwa ni wamiliki wa mashamba yaliyotwaliwa kutokulipwa fidia na kutopewa viwanja kama ilivyokuwa katika makubaliano na wengine kupewa viwanja katika maeneo ambayo hayajapimwa.

“Katika mgogoro huu Mkurugenzi wa TAA aliunda kamati ya uchunguzi na matokeo ameonyesha kuwapo  ukiukwaji mkubwa wa taratibu na ndiyo kuwa chanzo cha migogoro,” alisema Mjema.

Aliitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa haraka ili haki iweze kutendeka na wahusika kuchukuliwa hatua stahiki.

Alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuvilinda viwanja vingine 212 nilivyopimwa kwa ajili ya huduma za jamii vilivyopo Kigilagila na Kipunguni.


from MPEKUZI

Comments