Angela Merkel atangaza kuachia ngazi 2021

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametangaza kuwa hatagombea tena uongozi wa chama chake cha Christian Democratic Union -CDU, na kwamba muhula wa sasa wa ukansela ambao ni wa nne madarakani utakuwa wa mwisho.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama chake jijini Berlin, ambapo amesema kuwa muda umewadia wa kufungua ukurasa mpya.

Merkel mwenye umri wa miaka 64 amekuwa mwenyekiti wa chama cha CDU tangu mwaka 2000, na Kansela wa Ujerumani tangu mwaka 2005 ambapo katika kipindi cha miaka 13 kama Kansela, amekuwa pia mwanasiasa maarufu barani Ulaya.

Aidha, Merkel amegusia mivutano ya ndani ya vyama vinavyounda mseto wa serikali anayoiongoza, ambayo imesababisha mzozo baada ya mwingine, na kuhitimisha kwamba taswira inayotoka katika serikali hiyo haikubaliki.

“Kwa uamuzi huu najaribu kuchangia katika kuiwezesha serikali ya Ujerumani kujikita katika juhudi za uongozi bora, suala ambalo wananchi wamekuwa wakidai, kitu ambacho ni haki yao, hatua hii vile vile inakwenda sambamba na azma ya serikali ya Ujerumani kufanya tathmini ya nusu muhula, kuhusu ilivyotekeleza majukumu yake, kama ilivyokubaliwa na vyama vya CDU, CSU na SPD katika mkataba wa kuunda serikali ya mseto.” amesema Merkel

Hata hivyo, mwanasiasa huyo wa Ujerumani ambaye alikuwa akichukuliwa kama mwanamke mwenye nguvu zaidi duniani, na mwenye kauli ya mwisho katika Umoja wa Ulaya, alianza kupoteza ushawishi baada ya uamuzi wake wa kuruhusu wakimbizi zaidi ya milioni moja kuingia nchini Ujerumani mwaka 2015.


from MPEKUZI

Comments