Waziri Mkuu: Wanajiosayansi Mna Wajibu Wa Kulinda Madini Yetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanajiosayansi nchini wawe walinzi wa kwanza wa rasilmali za madini, maji na mafuta bila kujali wako serikalini au kwenye sekta binafsi.

“Katika utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuwa wa kwanza kujua kinachoendelea katika sekta zote mnazohusiana nazo, yaani madini, maji na mafuta. Haijalishi unafanya kazi serikalini au shirika binafsi, wewe ni Mtanzania na una jukumu la kulinda rasilimali za nchi yako.” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jana mchana (Alhamisi, Septemba 27, 2018), wakati akifungua warsha ya siku sita yaJumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania iliyoanza leo kwenye hoteli ya New Dodoma, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ambaye amefungua warsha hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka wanajiosayansi hao kutoka Serikalini, taasisi binafsi na vyuo vya elimu ya juu wasishiriki kulihujumu Taifa kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wasaliti namba moja.

“Msijihusishe au kushiriki kulihujumu Taifa lenu kwani kwa kufanya hivyo, mtakuwa wasaliti namba moja. Hakikisheni mnakuwa mabalozi wa Serikali katika mashirika haya kwa kutoa elimu juu ya sheria zinazosimamia sekta hizi huku mkisisitiza umuhimu wa kufuata sheria za nchi zenye kusimamia rasilimali zetu adhimu,” amesema.

Amesema mbali ya kilimo, rasilmali miamba na madini ndivyo vyenye mchango mkubwa wa kukuza viwanda kote duniani na kwamba utaalamu wa jiosayansi una mchango mkubwa kwenye malighafi za viwandani, upatikanaji wa maji ya kutosha nchini, mafuta, gesi asilia na uzalishaji wa nishati kupitia jotoardhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wanajiosayansi hao waisaidie Serikali kutafuta vyanzo vya maji vya uhakika ili itumie kihalali fedha zinazotengwa kwenye uchimbaji visima vya maji na kuepuka upotevu wa fedha.

“Ni jukumu la wanajiolojia la kutuambia wapi maji yapatikana. Muandae utaratibu mzuri wa kutunza takwimu kuhusu kiwango cha maji, ni wapi maji yalipo na ujazo wake. Kwenye eneo hili tumepoteza fedha nyingi sana, tumepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri ili tutoe huduma za maji wananchi lakini kwa sababu hatukuwashirikisha wanajiosayansi, wachimbaji wameenda kuchimba visima na wakakosa maji, yakabaki mashimo tu bila maji. Mna jukumu kubwa la kuisadia Serikali ili itumie vizuri fedha inazozitenga kwa ajili ya maji kwa kubainisha wapi kuna maji, yako kiasi gani na yako umbali gani,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri wa Madini, Bibi Angella Kairuki amesema wizara hiyo inakusudia kuanzisha chombo maalum cha usajili cha kuwatambua wanajiosayansi kisheria kupitia Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini (Geoscientists Registration Board -GRB) kama ilivyo kwa wahasibu, wahandisi na mabaraza ya wasajili mbalimbali ili kukabiliana na wataalamu feki wa fani hiyo.

“Wizara ya Madini inategemea wanajiosayansi wawe wazalendo kwa Taifa kwa kutoa taarifa za kitaalamu zinazoendama na uhalisia ili kuondoa malalamiko yanayotokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu hasa wale wanaojifanya wataalamu ilhali wakijua wazi hawana utaalamu wa fani hii,” amesema.

Amesema azma ya Serikali ni kumaliza changamoto zinazoikabili sekta hiyo ya madini zikiwemo ukiritimba uliokuwa ukifanyika katika mlolongo mzima wa utoaji leseni, utafutaji na uzalishaji wa rasilmali madini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments