Rais Magufuli Ataka FlyOver ya TAZARA Ifungwe Kamera

Rais John Magufuli ameagiza kufungwa kamera katika daraja la juu ‘flyover’ la Mfugale  lililopo eneo la Tazara  lifungwe kamera ili kuwabaini watu watakaokiuka  taratibu za usalama barabarani.

Mbali na daraja hilo, pia ameagiza madaraja mengine makubwa yanayojengwa nchini kufungwa kamera.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 27, 2018 wakati akizindua  daraja hilo.

“Ili hata pale anapokuja mtu amelewa na kusababisha ajali tumjue ni nani hata kama atatelekeza gari lake hapo,” amesema.

“Tutengeneze vitu vizuri vitusaidie na si kutuletea matatizo mengine ambayo yanaweza kuzuilika.”

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametaka miradi yote ya ujenzi inayosimamiwa na DMDP iwekwe chini ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura).

“Tarura ilipitishwa na Bunge hatuwezi kuwa na chombo kingine kinachojitegemea wakati tulishakubaliana. Hivyo barabara, madaraja, mifereji inayojengwa yote iwe chini ya Tarura,” amesema.

“Na lengo la kufanya hivi ni kutaka kuhakikisha fedha zote zinazoelekezwa katika miradi zinatumika ipasvyo.”


from MPEKUZI

Comments