Mahakama yataka upelelezi kesi ya Seth, Rugemarila ukamilike

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mshtakiwa Harbinder Singh Sethi na James Burchard Rugemarila ijitahidi kukamilisha upelelezi ili hatma ya kesi hiyo iweze kujulikana.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema hayo leo Septemba 27, 2018 mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Baada ya wakili Kishenyi kueleza hayo, wakili anayemtetea Rugemarila, Didas Respicius ameeleza mahakamani hapo kuwa sera ya mahakama ni mashauri yasikilizwe na kutolewa maamuzi kwa wakati.

"Tunashangaa kila kesi inapokuja upande wa mashtaka unaomba tarehe ya kuitaja kesi kwa zaidi ya mwaka sasa, washtakiwa wanateseka mahabusu," amesema Didas mahakamani hapo.

Wakili Kishenyi amedai wataendelea na upelelezi ili pande zote mbili zipate haki sawa.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka ujitahidi kukamilisha upelelezi ili hatma ya kesi ijulikane kabla ya kutangaza kuiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11,2018 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya Dola 22.1 milioni na Sh 309 bilioni.


from MPEKUZI

Comments