Mageuzi Sekta ya Madini Yaongeza Mapato....Tanzania sasa ni ‘DONOR COUNTRY’ sekta ya Afya

Serikali  kupitia mradi kabambe wa ujenzi wa vituo vya afya ngazi ya kata, kwa mwaka huu tayari imekamilisha vituo 210 ndani ya mwaka mmoja kutoka vituo 115 vya afya tangu wakati wa Uhuru.

Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi kwa vyombo vya habari imesema, vituo hivyo vinawekewa vifaa vya kisasa vya upasuaji na wodi za kina mama na nyumba za watumishi kujengwa.

“Serikali haijawekeza katika hospitali kubwa bali kwa sasa huduma muhimu zinapelekwa kwa wananchi kwa kujenga Hospitali za Rufaa katika mikoa saba, hospitali za wilaya 67 zinajengwa mwaka huu (tangu Uhuru tuna hospitali 77 za wilaya). Sh bilioni 105 zimetengwa kwa hospitali za wilaya 67,” alisema.

Amesema uwekezaji mkubwa wa vifaa, wataalamu na majengo umefanyika hospitali za Muhimbili, Mloganzila, MOI, Bugando, Benjamin Mkapa na sasa tiba kubwa za upasuaji wa moyo, operesheni ya kuongeza uwezo wa kusikia, tiba za kisasa za mifupa, kupandikiza figo, kutenganisha watoto zinafanywa nchini.

“Wagonjwa kutoka nchi jirani wameanza kuja Tanzania kupata huduma za kibingwa zenye hadhi ya juu na bei rahisi. Tumekuwa “donor country,” nchi wahisani katika afya. (Nchi za Comoro, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, DRC, Zambia na wataalamu wa nje),” aliongeza.

Akizungumzia hali ya uchumi wa nchi, alisema umeendelea kuwa imara ukikua kwa asilimia 7.0 mpaka 7.1 kwa mwaka na ukiwa miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi duniani na Afrika kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kimataifa kama vile Jukwaa la Uchumi Duniani na taasisi mbalimbali za kimataifa.

Alisema kwa dunia Tanzania ni ya tisa na kwa Afrika ni ya tano kwa uchumi unaokua kwa kasi kama takwimu ya 7.0 itaingizwa kwenye ripoti zijazo.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa nchi, iliasisi mageuzi katika sekta ya madini ikiwemo kutunga sheria mbili mpya, kuanzisha mashauriano na Kampuni ya Barrick, kujenga ukuta Mirerani na kuzuia mabaki (kaboni) za dhahabu kusafirishwa na kuchakatwa nje ya mkoa zinakozalishwa.

“Kwa kutunga sheria mpya na kufanya mashauriano na Barrick, Tanzania imesifika duniani na nchi nyingine zimeanza kuiga….Wizara ilipanga kukusanya Sh bilioni 194.6 mwaka 2017/18, lakini ikakusanya zaidi yaani Sh bilioni 301.6 ambayo ni zaidi ya asilimia 55 ya lengo,” alifafanua.

Amesema Septemba 20, 2017 Rais John Magufuli aliagiza kujengwa ukuta Mirerani na Aprili mwaka huu ulikamilika ukiwa na eneo la mraba la kilometa 24.5 na mapato yameongezeka kutoka kilo 164.6 zenye thamani ya Sh milioni 71.8 mwaka 2016 hadi (Januari -Juni, 2018 pekee) kilo 449.6 zenye thamani ya Sh milioni 893.8.

Amesema Wizara ya Madini inaendelea na mageuzi mbalimbali ikiwemo kujenga vituo saba vya umahiri vitakavyokamilika Desemba mwaka huu kwa thamani ya Sh bilioni 11.9 kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo na utaalamu zaidi wa uchimbaji.

Aidha, alisema vituo vinne vya mfano pia vitajengwa kwa thamani ya Sh bilioni 5.2 kuwasaidia wachimbaji kupata teknolojia rahisi ya uchenjuaji wa madini na kuyaongezea thamani.

Dk Abbasi amesema serikali inatumia fedha za ndani kugharamia elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne ambapo Sh bilioni 23.85 zinatumika kila mwezi ikiwemo gharama za uendeshaji wa shule na elimu ya juu utaratibu mpya na wenye ufanisi wa mikopo umeondoa kero za wanafunzi kugomagoma.


from MPEKUZI

Comments