Na Felix Mwagara, MOHA-Buhigwe
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameitaka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma ishirikiane na Jeshi la Polisi kufanya operesheni maalum ya kuwaondoa wahamiaji haramu mkoani humo.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika uwanja wa Mnanila mjini Manyovu wilayani Buhigwe, leo, Lugola alisema anataarifa za kutosha kuhusu wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani wapo mkoani humo, hivyo lazima waondolewe kwa mujibu wa sheria.
Lugola ambaye alikua akishangiliwa na wananchi baada ya kutoa agizo hilo, pia alikemea tabia ya baadhi ya watu wanaohifadhi raia hao wa kigeni ambao wameingia nchini kinyume cha sheria.
“Sasa natoa agizo hili na litekelezwe, Uhamiaji mkoa washirikiane na polisi kuwaondoa raia hawa wa kigeni ambao wameingia nchini kwa njia zisizo halali, nataka operesheni hii ianze mara moja,” alisema Lugola.
Lugola pia aliirudia kauli hiyo ya kuondolewa kwa wahamiaji hao haramu alipokua anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya Kigoma Vijijini, na kuongeza kuwa anashangaa wahamiaji hao wanaendelea kuwepo mitaani huku maafisa uhamiaji wakiwepo mkoani humo.
“Hivi inakuaje, wananchi wanalalamika hapa kuhusu uwepo wa wahamiaji haramu, lakini Uhamiaji mpo, mnakaa kimya tu, mnataka mpaka mimi nije ndio nitoe maelekezo haya? Hii sitaki kusikia tena, nataka operesheni hii ianza mara moja na iwe endelevu,” alisema Lugola.
Hata hivyo, Lugola alisema katika operesheni hiyo lazima maafisa wa uhamiaji wawe makini wakati wanawaondoa wahamiaji haramu pekee na sio kuwasumbua wananchi wa Kigoma ambao ni raia halali wa nchi hiyo.
Lugola alifafanua kuwa operesheni hiyo itasaidia kupunguza matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali mkoani humo ambapo kwa kiasi kikubwa hutekelezwa na wahamiaji hao haramu.
Aidha, Waziri Lugola akiwa wilayani Buhigwe, pia ametembelea kituo cha Polisi cha Manyovu kilichopo mpakani na nchi ya Burundi na kukagua utendaji kazi wa askari Polisi wa kituo hicho pamoja na kuiwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu kujua makosa yaliyowafanya wawepo ndani ya kituo hicho.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment