Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold imekubali kuinunua Kampuni ya Randgold ya Afrika Kusini ambayo ni mshindani wake mkubwa kibiashara.
Barrick ndiyo mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Plc ikiwa na umiliki wa asilimia 64 ya hisa.
Wakati mpango wa ununuzi wenye thamani ya Dola bilioni sita za Marekani ukikamilika, Ofisa Mtendaji Mkuu mpya wa kampuni mpya itakayozaliwa, Mark Bristow, ameonyesha nia ya kumaliza mgogoro kati ya Acacia na Serikali ya Tanzania.
Huku wachambuzi wa sekta ya madini wakisema uzoefu wake muda mrefu katika biashara ya madini barani Afrika utasaidia kufanikisha majadiliano kati ya Acacia na Serikali ya Tanzania.
Bristow alinukuliwa na gazeti la Financial Times akisema: “Tuna fursa kubwa ya kufanya kazi na Acacia kwa kutafuta suluhisho ili kutengeneza thamani na uwazi zaidi kwa Tanzania.”
Tangu Acacia ilipozuiliwa kusafirisha makinikia nje ya nchi, hisa zake zimeanguka kwa zaidi ya asilimia 75.
Pia wachambuzi hao walisema uamuzi wa Barrick kumnunua mshindani wake ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo ya Canada kujitutumua kwa kuwa wawekezaji wengi waliikimbia kutokana na miaka mingi ya matumizi makubwa na faida ndogo.
Kutokana na ununuzi huo, Barrick itakuwa kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu duniani ikiwa na mtaji wenye thamani ya Dola bilioni 18 za Marekani utakaotumika kuendeshea miradi yenye faida kubwa Afrika na Marekani.
Hata hivyo, uzalishaji wa dhahabu kwa Barrick umekuwa si mzuri kutokana na kuanguka kutoka ‘ounce’ milioni nane katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kufikia ‘ounce’ milioni 5.3 kwa sasa.
Taarifa za masoko zinaonyesha hisa za Barrick zimeanguka kwa asilimia 30 mwaka huu wakati zile za Randgold zikianguka kwa kiasi hicho hicho huku ikikabiliwa na matatizo mengine kama mgomo katika mgodi wake mkubwa na sheria mpya za madini nchini Congo.
Kwa mujibu wa Financial Times, kampuni hiyo mpya inatarajia kuzalisha ‘ounce’ milioni 6.5 za dhahabu kwa mwaka na kumpiku mshindani wake mkubwa Kampuni ya Newmont Mining ya Marekani huku ikiandikishwa katika Soko la Hisa la Toronto nchini Canada na New York nchini Marekani.
“Sekta yetu imekuwa ikilaumiwa kutokana na kuwa na malengo yasiyolenga mbali, ukuwaji usioridhisha na faida ndogo,” alisema na kuongeza Bristow ambaye ni Mkurugenzi na mwanzilishi wa Randgold:
“Kampuni mpya inayozaliwa itakuwa tofauti tukiwa na malengo ya muda mrefu na kutengeneza faida nzuri. Ili kufika tunapotaka lazima tuangalie upya na kwa umakini mali zetu, namna tunavyofanya biashara na kufanya uamuzi mgumu pale inapobidi.”
Kampuni hiyo mpya itamiliki na kuendesha migodi mikubwa zaidi duniani na yenye kutengeneza faida nzuri ikiwa ni pamoja na Mgodi wa Cortez na Goldstrike ya Nevada, Marekani, Kibali wa Congo na Luo-Gounkoto uliopo nchini Mali.
“Kipimo cha mafanikio yetu itakuwa ni faida tunayozalisha na sio ounce tunazozalisha,” alisema John Thornton ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick.
Credit: Mtanzania
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment