Wizara ya afya Yatuma Mtaalum BINGWA Kuchunguza mwili wa mwanafunzi aliyeuawa Kwa Kichapo na Mwalimu

Na WAMJW
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemwagiza mtaalamu bingwa wa uchunguzi kwenda mkoani Kagera kwa ajili ya kurejea uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius (13) wa shule ya Msingi Kibeta iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera na kuwahakikishia wanafamilia na wananchi kuwa uchunguzi utafanyika kwa ufanisi na haki itatendeka. 

Ameyasema hayo mapema leo wakati akizungumzia kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo kinachosemekana kilisababishwa na mwalimu wake Respicius Patrick baada ya kumpiga kwa kumtuhumu kumuibia pochi yake.

Waziri Ummy amesema kuwa kitendo hicho ni cha ukatili kwani ni kinyume na Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 13 (2) ambayo inasisitiza kutolewa kwa adhabu stahiki kwa mtoto kulingana na umri, hali ya kimwili na kiakili.

Aidha, amelaani vikali Vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto vinvyoendelea kufanyika katika jamii na kusema kuwa Serikali itahakikisha inawafuatilia na kuwachukulia hatua watakaofanya vitendo hivyo.

Ameongeza kuwa wa kuwa suala hilo lipo mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi, anaamini pindi uchunguzi utakapokamilika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa.

Amesisitiza kuwa jamii na kila mtu anaowajibu wakuhakikisha mtoto anaishi, kukua na kuendelezwa katika mazingira salama na rafiki kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.


from MPEKUZI

Comments