Uongozi wa Viwanja vya Ndege vya Songwe na Kigoma, umejiandaa kwa kushirikiana na maafisa afya, kuhakikisha hakuna mgonjwa mwenye dalili za Ebola anaingia nchini, akitokea maeneo ya Tunduma na nchini Burundi.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Bw. Pius Kazeze alimwambia Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi.Bahati Mollel kwa njia ya simu kuwa, tayari Maafisa wa Afya wameshafunga mashine maalum (thermo scanners) inayotambua joto la mwili la abiria ambaye anasafiri kwa kupitia kiwanja hicho, na likizidi 38 anatakiwa kutoa taarifa za afya yake.
Bw. Kazeze amesema Kiwanja cha Songwe ni tofauti kidogo na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo zaidi wanakagua abiria wanaoondoka kwa kuwa wengi wanatoka mpakani maeneo ya Tunduma na kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Tayari maafisa Afya wamefunga mashine ya ukaguzi wa afya eneo la nje la kuondokea abiria kwani kwetu huku tunapata abiria wengi wanaotoka nchi jirani wanaopitia mpakani Tunduma, hivyo wengi wao wanatoka nchi zinazopakana na Kongo, ambayo inasadikika ugonjwa wa Ebola umeibuka kwa kasi kubwa,” alisema Bw. Kazeze.
Hatahivyo, amesema mbali na mashine hiyo kubwa iliyowekwa sehemu maalum, pia wanamashine mbili ndogo zinazotumiwa kwa kushikwa mkononi na maafisa Afya, lakini wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa Watumishi wa afya, ambao tayari wameshaomba kuongezewa mmoja ili kufanikisha kazi hiyo kuwa rahisi.
Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Bw. Theophan Bileha amesema wapo mbioni kiweka kifaa hicho kwa kuwa wanatarajia abiria kutoka Burundi watakaowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), itakayoanza safari zake kuanzia Agosti 30, 2018.
“Tumeshafanya kikao na wenzetu wa Afya, na wameahidi kuleta mashine mojawapo, tunatarajia abiria wanaotoka Bujumbura, kwani tumeambiwa ATCL itaanza kwenda huko kuanzia tarehe 30, na hawa wapo watakaoshuka hapa na wengine wanakwenda kwenye viwanja vingine kulingana na ratiba ya ndege hii,” alisema Bw. Bileha.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma, Dk. Peter Nsanya amesema mashine hiyo itawekwa kiwanjani hapo kwa kipindi, ambacho ndege zinatua na baada ya ratiba za ndege kumalizika, wanahamishia eneo la Bandarini kwa kuwa pia kuna abiria wanaotoka maeneo mbalimbali.
“Sisi tumejipanga kukabiliana na maradhi haya ikiwa na kuhakikisha hatutaruhusu uingie nchini, na ndio maana tunaratiba za ndege, ambapo tutakuwa tunakwenda kutoa huduma, na baadaye kuhamia bandarini,” amesema.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Mohamed Maulid amesema wamejiandaa kwa kushirikiana na Maafisa Afya wamekuwa wakitumia mashine ya mkono kwa ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi za Uganda, Nairobi na Kongo.
Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha vifo.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele na kutokwa damu.
Juzi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kilitangaza kuchukua hatua kali za kuweka zuio kwa abiria wanaongia nchini kupitia Kiwanja hicho, ambapo kumefungwa vifaa ambavyo vinabaini joto la abiria na endapo litazidi nyuzi joto 38, atatakiwa kutoa maelezo zaidi ya maisha yake.
Pia abiria wote wanaowasili kwa ndege zinazotoka nchi jirani na Kongo wanatakiwa kupitia eneo maalum ambalo hutakiwa kunawa mikono yao kwa dawa maalum ili kuua vijidudu mbalimbali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO CHA MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment