Anna Mghwira Akabidhiwa Rasmi Kadi ya CCM

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemkabidhi rasmi kadi ya uanachama wa chama hicho mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye alijiunga na chama hicho Desemba 2017.

Mghwira alijiunga na CCM, Desemba 8, 2017  katika mkutano wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), mjini Dodoma akitokea Chama cha ACT-Wazalendo, mkutano ambao Rais John Magufuli alikuwa mgeni rasmi.

Tangu wakati huo, alikuwa hajakabidhiwa rasmi kadi ya uanachama, hadi jana jioni Jumatano Agosti 29, 2018 alipokabidhiwa kadi ya uanachama na viongozi wa CCM kata ya Kilimanjaro, kata ambayo ndio anaishi.

Viongozi waliomkabidhi kadi hiyo ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Kilimanjaro, Ernest Mlembezi, Diwani wa kata hiyo, Priscus Tarimo na Katibu wa tawi la Mawenzi, Joyce Mchome..

Mghwira ambaye alikuwa mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, aliwahi kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, ambapo Rais John Magufuli aliibuka mshindi.

Juni 3, 2017, Rais Magufuli alimteua kuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, kuchukua nafasi ya Said Meck Sadiki ambaye alitangaza kustaafu.


from MPEKUZI

Comments