Waziri Mkuu: Michikichi Ni Zao Kuu La Sita La Biashara Nchini


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imelitangaza zao la michikichi kuwa zao kuu la sita la biashara linalotarajiwa kuinua uchumi Taifa.

Awali, kulikuwa na mazao makuu matato ya biashara nchini ambayo ni korosho, tumbaku, pamba, kahawa na chai, ambayo yanategemewa na Taifa kukuza uchumi.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 29, 2018) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mwakizega wilayani uvinza mkoani kigoma.

Alisema baada ya Serikali kupata mafanikio katika mazao ya korosho, tumbaku, pamba, kahawa na chai, sasa imeamua kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma ili lianze kuzalishwa kwa wingi na kuongeza pato la serikali.

“Tulianza na mazao matano, baada ya wakulima wake kupata faida sasa tumehamia  katika mazao mengine likiwemo la michikichi,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.

Alisema kwa mwaka Serikali inatumia zaidi ya sh. bilioni 600 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, hivyo ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha.

Waziri Mkuu aliwaagiza wananchi wa mkoa wa Kigoma kuandaa mashamba ya kupanda michikichi wakati Serikali ikipanga namna ya kuwasambazia mbegu.

Pia aliwaagiza wananchi wote wapande michikichi mbele ya nyumba zao kama mapambo ambayo baada ya miaka mitatu itageuka na kuwa chanzo cha mapato.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea na kukagua shamba jipya la michikichi la kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 821 KJ Bulombora.

Akiwa katika shamba hilo jipya lenye ukubwa wa ekari 34, Waziri Mkuu alipata fursa ya kupanda mche wa mchikichi kwa lengo la kuhamasisha kilimo cha zao hilo.

Alisema Serikali itahakikisha inafuatilia kwa ukaribu kilimo cha zao hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa shamba hadi upatikanaji wa pembejeo.

Kadhalika,Waziri Mkuu aliwaagiza wazazi kuwakatia vijana wao maeneo kwa ajili ya kilimo cha michikichi, jambo litakalowakwamua kiuchumi badala ya kuwa tegemezi.

Pia aliwashauri vijana hao na wakulima wengine wajiunge katika vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo na kuendeleza mashamba yao ya michikichi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments