Wabunge Wa Kigoma Waridhishwa Na Utendaji Wa Serikali ......Waipongeza kwa kampeni ya kuhamasisha kilimo cha michikichi
WABUNGE wa mkoa wa Kigoma wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi kwa sababu litasaidia kuondoa umasiki kwa wananchi wa mkoa huo.
Wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba Serikali kulifufua zao hilo kwa kuwa ndilo zao kubwa la biashara linalotegemewa na wananchi wengi wa mkoa huo, hivyo kitendo cha kuanzisha kampeni hiyo kinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kuwakwamua wananchi.
Wakizungumza kwa jana (Jumamosi, Julai 28, 2018) wabunge hao waliahidi kushirikiana na Serikali bega kwa bega kuhakikisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi linafanikiwa kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Wabunge hao waliyasema hayo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma. Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau wa zao hilo.
Miongoni mwa wabunge hao ni mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye aliipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrfu cha wananchi wa mkoa huo cha kufufuliwa kwa zao la michikichi kwa kuwa litakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Kigoma.
“Nakupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa kitendo hiki cha kufufua zao la michikichi kwani hiki ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigoma kwa hatu hii naamini kuwa leo hata waliotangulia mbele ya haki watakuwa wanatabasamu huko waliko,”.
Pia mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi na viongozi wa mkoa wa Kigoma kuwa ni vema wakashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha zao hilo linafufuliwa kwa watu kuchangamkia fursa ya kupanda michikichi kwenye mashamba yao.
Mbunge mwingine wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba alisema changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa mkoa huo ni upatikanaji wa mbegu bora za michikichi, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia katika upatikanaji wa mbegu.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Trade Mark Bw. John Luaga alisema walifanya utafiti kuhusu zao la michikichi na walibaini kuwa kuna soko kubwa la mafuta ya mawese ndani ya nchi yetu, pamoja na nchi za jirani ila uzalishaji wa mafuta hayo ndani ya nchi bado ni mdogo sana.
Alisema hali inachangiwa na kuwepo kwavikwazo vichache vinavyokwamisha ongezeko la uzalishaji wa ndani, ambavyo ni matumizi ya teknologia hafifu katika kilimo cha mchikichi, na ukamuaji wa mafuta ya mawese.
Pia ukosefu wa miundombinu na usafiri, ukosefu wa maghala ya kukusanyia matunda ngazi ya wilaya, na badala yake mkulima mmoja mmoja anahangaika kupeleka kwa mteja hivyo kumuongezea gharama, ukubwa wa gharama za usafiri kutoka shambani mpaka sokoni.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Josephat Faustine alisema kilimo cha zao la michikichi kina faida kubwa na kinawekezeka, hivyo wao wataanisha maeneo yote yanayofaa kuwekeza.
Pia Mkurugenzi huyo wa TADB alisema benki yao inauwezo wa kutoa mikopo ya mitaji kwa vituo vya uzalishaji mbegu za zao la michikichi na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mbegu, hivyo ni muhimu kwa wakala wa mbegu kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kufufua zao hilo na kwamba changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la michikichi ikiwemoya upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa ajili ya kununua mbegu au miche mipya zinafanyiwa kazi.
Waziri Mkuu alisema Serikali itahakikisha zao hilo linafufuliwa na kulimwa kwa wingi mkoani Kigoma pamoja na mikoa mingine inayolima michikichi nchini, ambapo amewata Maafisa Kilimo katika ngazi zote waanzishe mashamba ya michikichi.
Pia amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchi kuhakikisha mashamba ya wananchi yanapimwa na wahusika kupewa hati ili ziwaweze kupata dhamana ya mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha na kuwekeza kwenye kilimo.
Waziri Mkuu alisema halmashauri zinazolima michikichi viongozi wake wantakiwa kuanzisha vitalu vya miche ya zao hilo na watakaoshindwa kuanzisha vitalu hivyo pamoja na kuhamasisha kilimo cha michikichi kwenye maeneo yao wajitathimini mwenyewe.
Aliongeza kuwa kuanzia sasa mkoa huo uhakikishe miche ya michikichi inapandwa katika maeneo yote yakiwemo ya pembezoni mwa barabara, katika mashamba ya shule za msingi na sekondari, kambi ya JKT na kwenye magereza na kwenye makazi ya wananchi.
Hata hivyo Waziri Mkuu alitoa angalizo kwa wawekezaji watakaowekeza katika kilimo cha michikichi kutoanzisha migogoro na wananchi watakaowakuta katika maeneo yao na badala yake washirikiane nao vizuri kwa sababu migogoro haina tija kwao na kwa wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment