TFDA Yatakiwa Kusajili Jengo La Uzalishaji Chakula Ndani Ya Siku 10.

NA WAMJW- DAR ES SALAAM.
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kutoa kibali cha kusajili jengo la kuzalisha bidhaa za chakula ndani ya siku kumi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha wadau kujadili mchango Taasisi za Serikali katika kuanzisha na kuboresha viwanda vya Chakula nchini leo jijini Dar es salaam.

"Naielekza TFDA kutoa kibali cha kusajili jengo la kutengeneza bidhaa za chakula ndani ya siku 10 pamoja na siku 30 za kusajili bidhaa husika ili kuleta chachu ya maendeleo ya viwanda nchini" alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy ameitaka TFDA kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za vyakula kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ya sayansi juu ya uzalishaji bora wa vyakula na wenye tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amewataka TFDA kutopunguza viwango vyao vya ukaguzi wa bidhaa za vyakula ili kuleta sifa na ushindani kwenye soko la kimataifa.

"Nazitaka Taasisi za Serikali ikiwemo TFDA, TBS, MKEMIA MKUU WA SERIKALI na taasisi ya Mionzi kushirikiana katika kudhibiti ubora wa bidhaa nchini na kupunguza vikwazo kwa wawekezaji wa viwanda vya chakula nchini" alisema Waziri Mwijage.

Aidha Waziri Mwijage amewataka wajasiliamali wasibweteke katika kutengeneza bidhaa zinazokidhi viwango kwa mahitaji na zenye kulinda afya za watanzania.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bi. Agness Sitta Kijo amesema kuwa wamejidhatiti kuhakikisha hawatokuwa vikwazo kwa wawekezaji katika sekta ya uwekezaji kwenye viwanda vya chakula nchini.

Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania Dkt. Edward Sembeye ameipongeza TFDA kwa kupunguza malalamiko na vikwazo vingi kwa wajasiliamali na wawekezaji wadogo wa vyakula hapa nchini.

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments