Serikali imetangaza kunyanganya leseni za uchimbaji madini ambazo hazitumiki kwa muda mrefu pamoja na vitalu ambavyo vimehodhiwa na wachimbaji bila kuendelezwa wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Pia imewataka wachimbaji wote wa madini ya dhahabu wanaofanya shughuli zao kwenye vyanzo vya maji na kuharibu mazingira kuondoka mara moja.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo jana Jumatatu Julai 30 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Chunya ikiwa ni siku yake ya siku kufanya ziara kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.
“Ndugu zangu tumesikia hapa kwamba kulikuwa na shughuli za uchimbaji madini kwenye vyanzo vya maji na kama mnavyojua uchimbaji madini unatumia madawa kadhaa ambayo wakisafisha yanaingia ndani ya mto.
“Sasa vile vimelea vikiingia kwenye maji yale sio rahisi kusafishwa vikaondolewa na Chunya vyanzo vya maji ni vichache na ndio maana tumefunga migodi yote ambayo imekuwa ikifanya shughuli zake kwenye vyanzo vile. Nasisitiza tena shughuli zozote zinazofanyika kule mtoni za kuharibu maji, za kuharibu vyanzo vya maji zisimame mara moja na waondoke, hatutawavumilia hawa watu,” alisema Samia.
Awali, Waziri wa Madini, Angela Kairuki amesema kuna watu wamepewa leseni za uchimbaji wa madini lakini hawaziendelezi wala vitalu walivyopewa pia hawaviendelezi watazinyang’anya leseni hizo na kuwapatia wengine wenye uhajitaji.
Alisema hilo linakuja baada ya malalamiko ya wachimbaji wadogo ambao hawana maeneo ya kuchimba madini lakini maeneo makubwa yamehidhiwa na wachimbaji wakubwa ambao hawayaendelezi.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, wapo watu wamepewa leseni za uchimbaji madini lakini lakini hawazitumii leseni hizo, hawajaendeleza maeneo ya uchimbaji ambayo wamepewa na kwa kuwa wilaya hii (Chunya) imejikita zaidi kwenye uchimbaji madini niseme katika hadhara hii tunawapa onyo la mwisho wale wote tuliowapa leseni lakini hawaziendelezi tutazifuta na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuwekeza.”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment